Leo ni siku ya Jumapili, Machi 4, 2018.

Jumapili, Machi 4, 2018Leo ni Jumapili tarehe 15 Jamadith-Thani mwaka 1439 Hijiria, mwafaka na tarehe 4 Machi, mwaka 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1403 iliyopita yaani sawa na tarehe 15 Jamaduth-Thani mwaka 36 Hijiria, kwa mujibu wa baadhi ya wanahistoria, vilianza vita vya Jamal, baina ya jeshi la Imam Ali (as) na kundi la wafanya vurugu na fitina. 
Katika vita hivyo, jeshi la Kiislamu lililishinda kundi hilo ambalo lilianzisha uasi baada ya kushindwa kustahmili uadilifu wa Imam Ali, na hivyo kuamua kuvunja baia.
Viongozi wa kundi hilo ambalo lilifahamika kwa jina la Nakithina yaani wavunja ahadi, walikuwa Twalha na Zubair ambao awali walielekea mjini Makkah kutoka Madina kwa ajili ya kukusanya jeshi kubwa na kulichochea kwa matarajio ya kufikia malengo yao batili ya kutaka kutwaa utawala kwa nguvu. 
Baada ya kukusanya jeshi hilo, walielekea mjini Basra, Iraq. 
Ili kuzuia fitina hiyo, Imamu Ali (as) alilifuata kundi hilo na hatimaye majeshi ya pande mbili yakakutana na kupambana vikali karibu na mji huo wa Basra, kusini mwa Iraq ya leo. 
Awali mtukufu huyo alijitahidi kuhakikisha mgogoro huo unamalizika kwa njia ya amani bila kutokea vita na ni kwa ajili hiyo ndio maana alifanya mazungumzo na upande wa pili kwa muda wa siku kadhaa. 
Kwa kuzingatia kuwa upande wa adui uliamini kuwa ungeibuka na ushindi katika vita hivyo, ulikataa njia ya amani na hivyo kuingia vitani ingawa hata hivyo ulishindwa vibaya na jeshi la Imam Ali (as).
Siku kama ya leo miaka 668 iliyopita, sawa na tarehe 15 Jamadu Thani mwaka 771 Hijria, alifariki dunia Muhammad bin Hassan Hilli, maarufu kwa jina la 'Fakhrul Muhaqqiqiin', faqihi na msomi mkubwa wa Kiislamu. 
Mwanachuoni huyo alizaliwa mwaka 682 Hijria na kupata elimu ya kidini kutoka kwa baba yake mzazi, Allamah Hilli na wanachuoni wengine wa zama zake. 
Fakhrul Muhaqqiqiin ameacha vitabu vingi na miongoni mwavyo ni Manbaul Asrar na Tahswilul Najah.
Na siku kama ya leo miaka 161 iliyopita, mji wa Herati wa kaskazini magharibi mwa Afghanistan ya leo, ulijitenga na Iran. Mji huo na viunga vyake, isipokuwa kwa vipindi vifupi, ulikuwa sehemu ya Iran. 
Hata hivyo kufuatia kuongezeka upenyaji wa Uingereza katika eneo la bara Hindi, wakoloni hao waliichochea serikali ya mji huo ili ijitenge na Iran na katika uwanja huo, mtawala wa Kabul na Qandahar aliuvamia mji wa Herat na kuudhibiti. 
Hata hivyo katika kipindi cha utawala wa mfalme Naser al-Din Shah Qajar wa Iran, jeshi la nchi hii liliuzingira mji huo wa Herat na mwaka 1235 Hijiria Shamsia likafanikiwa kuurejesha katika himaya ya Iran. 
Katika uwanja huo, serikali ya kikoloni ya Uingereza ambayo ilikuwa inaelekea kushindwa, ilieneza askari wake katika maeneo ya kusini mwa Iran na kudhibiti miji kadhaa baada ya kujiri mapigano makali kati ya pande mbili. 
Baada ya hapo Ufaransa ilikuwa mpatanishi kati ya Uingereza na Iran ambayo wakati huo ilikuwa haina nguvu ya kukabiliana na askari wa mkoloni Mwingereza. 
Kufuatia hali hiyo hatimaye Iran ililazimika kukubali mkataba wa Paris kwa kuiacha Herat na maeneo mengine ya viunga vyake kuweza kujitenga na Iran.
Hii nikwahisani ya parstoday.

Comments