Hizam al Assad ameeleza kuwa kurefushwa muda wa vikwazo kumetekelezwa sambamba na kuendelea na kushtadi mashambulizi ya muungano vamizi wa Saudia huko Yemen; muungano ambao kila uchao unaishambulia Yemen na kutenda uhalifu na jinai kubwa zaidi dhidi ya raia wa nchi hiyo.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Jumatatu iliyopita lilipitisha azimio la kuongezwa muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Yemen hadi mwezi Februari mwaka 2019.
Saudi Arabia ilianzisha uvamizi wa kijeshi huko Yemen mwezi Machi mwaka 2015 kwa uungaji mkono wa Marekani na Uingereza na kisha kuizingira nchi hiyo katika mipaka ya majini, nchi kavu na baharini.
Ni karibu miaka mitatu sasa ambapo Saudia, ikiwa ni nchi ya Kiislamu na Kiarabu, inaendelea kuwaua wananchi madhulumu wa Yemen kwa kutumia silaha za kisasa zaidi na za maangamizi makubwa kutoka Marekani, Uingereza na baadhi ya nchi nyingine za Magharibi.
Hata hivyo matukio ya huko Yemen yanaonyesha kuwa Saudi Arabia imefeli kufikia malengo yake kwani utawala wa Aal Saud ulidhani kwamba katika muda wa miezi miwili au mitatu ungeweza kufanikisha malengo yake ya kibeberu huko Yemen.
Ni wazi kuwa leo hii baada ya kupita karibu miaka mitatu ya mgogoro huo wa kulazimishwa dhidi ya wananchi wa Yemen, tunashuhudia kugonga mwamba kikamilifu Saudi Arabia katika uvamizi wake huo dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Kuhusiana na suala hilo tovuti ya habari ya al Badil ya Misri imemnukuu Khalid Abdulmuneim na kuandika kuwa: Vita vya Saudia dhidi ya Yemen vinaingia katika mwaka wake wa nne huku Riyadh ikiwa imeambulia patupu huko Yemen; ni idadi ya vifo na maafa tu yanayaosababishwa na vita hivyo ndiyo yanayoongezeka kila uchao.
Wale wote ambao hawajauliwa kwa silaha za Marekani na Uingereza hivi sasa wanaangamia kufuatia kuzingirwa kidhulma Yemen na kuenea ugonjwa wa kipindupindu kote nchini humo, yote hayo yakiwa ni natija ya vita vikubwa na kuzingirwa pande zote Yemen.
Hayo yote yanajiri huku serikali za Magharibi zikiendeleza ukandamizaji wao mkubwa dhidi ya wananchi wa Yemen. Serikali za Magharibi kwa kiburi kabisa zinasisitiza kuendeleza uungaji mkono wao kwa utawala vamizi wa Aal Saud. Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) hivi karibuni ilisisitiza waziwazi kwamba itaendelea kuunga mkono muungano vamizi wa kijeshi wa Saudia katika vita dhidi ya Yemen.
Pentagon imekiri kuwa, itaendelea kuiunga mkono Saudia kwa kutoa huduma za nishati na mafuta kwa ndege za kivita za utawala huo sambamba na kuupatia taarifa za kiintelijinsia muungano huo vamizi wa kijeshi.
Hii ni katika hali ambayo kwa mashinikizo ya nchi za Magharibi, badala ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwaunga mkono wananchi walioathirika na vita na walio chini ya mzingiro wa Yemen na kuchukua hatua za kusitisha vita hivyo vya kidhulma vya Saudia dhidi ya wananchi hao limekuwa likichukua maamuzi na misimamo dhaifu na ya kulegalega kuhusu matukio ya kieneo khususan ya nchini Yemen.
Katika mazingira kama hayo, hatua ya kuiwekea Yemen vikwazo mbalimbali vikiwemo vya silaha inaweza kuwa na maana gani ghairi ya kuwa bega kwa bega na Saudi Arabia katika kuwauwa zaidi wananchi wa Yemen? Siasa za kuwawekea wananchi wa Yemen vikwazo vya silaha zinatekelezwa huku raia hao wakiwa wamezingirwa na kuandamwa na jinai za kila aina za utawala wa Aal Saud; hatua ambayo ni sawa na kuubariki utawala wa Aal Saud uendeleze mauaji zaidi ya kuteketeza roho za raia wa Yemen.
Utendaji kama huo unakinzana na masuulia ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo maamuzi yake yanapasa kuwa katika fremu ya kusaidia kurejesha amani na usalama duniani na kusitisha vita katika uga wa kimataifa.
chanzo:parstoday.
Comments