Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji na viongozi wengine wa chama hicho
wameripoti Kituo Kikuu cha Polisi leo asubuhi Machi 5, 2018.
Februari
27, 2018 viongozi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe ambaye leo hayupo kwa maelezo kuwa ni mgonjwa, walifika kituoni
hapo na kuhojiwa kwa takribani saa tano, kisha kuachiwa kwa dhamana na
kutakiwa kuripoti tena leo.
Viongozi
hao wakiongozwa na Dk Mashinji ambaye Februari 27, 2018 hakufika
kuhojiwa kutokana na kuwa nje ya nchi, mpaka saa 2:15 asubuhi walikuwa
wamewasili wote kituoni hapo.
Mbali na Mashinji, viongozi wengine waliofika kituoni ni naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).
Pia,
wamo mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee;
mwenyekiti wa kanda ya Serengeti, John Heche na Esther Matiko ambaye ni
mweka hazina wa Bawacha.
Viongozi hao wameambatana na wakili Frederick Kihwelo na Alex Massaba pamoja na Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya.
Massaba amesema kuwa Mbowe hatoweza kufika kwa kuwa ni mgonjwa.
Februari 20, 2018 Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam iliagiza kukamatwa viongozi saba waandamizi wa Chadema akiwamo Mbowe.
Wito
huo ulikuja siku chache baada ya tukio la kuuawa kwa mwanafunzi wa Chuo
cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.
Akwilina
aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni,
Kinondoni jijini Dar es Salaam wakati polisi wakiwatawanya wafuasi wa
Chadema waliokuwa wakienda ofisi za mkurugenzi wa Halmashauri ya
Kinondoni kudai viapo kwa mawakala wao.
chanzo:mpekuzi.
Comments