Siku kama ya leo miaka 1114 iliyopita kisiwa cha Malta maarufu kama "Herini ya Mediterania" kilitwaliwa na Waislamu na kuunganishwa na mamlaka ya nchi za Kiislamu.
Utawala wa Waislamu wa kisiwa cha Malta uliendelea hadi mwaka 1091 yaani hadi zama za udhibiti wa kaumu ya Norman kisiwani humo.
Malta ambayo inaundwa na visiwa vingi vidogo na vikubwa ina ukubwa wa kilomita mraba 316 na jamii ya watu karibu nusu milioni.
Siku kama ya leo miaka 1048 iliyopita, alifariki dunia mtaalamu wa mashairi wa Kiislamu kwa jina la Ibn Hajjaj.
Ibn Hajjaj alizaliwa mjini Baghdad, Iraq ambapo akiwa kijana alijikita katika taaluma ya mashairi na kutokea kuwa maarufu katika uwanja huo.
Miongoni mwa athari za malenga huyo ni pamoja na kitabu cha juzu kumi ambapo baadhi zipo katika maktaba za mjini Baghdad.
Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, mgogoro mkubwa katika ngazi za uongozi wa Urusi ya zamani ulifikia kikomo kufuatia kutangazwa kifo cha Konstantin Chernenko na badala yake Mikhail Gorbachev ambaye wakati huo alikuwa mwanachama kijana zaidi katika ofisi ya kisiasa ya chama cha Kikomunisti akatangazwa kuchukua nafasi ya Chernenko.
Hatua ya kuchaguliwa Gorbachev kuongoza chama hicho cha Kikomunisti ilikwenda sambamba na kujiri mabadiliko makubwa, ambayo hatimaye yalipelekea kusambaratika Umoja wa Kisovieti.
Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Haj Agha Hussein Khadimi, faqihi, alimu na mujtahidi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu.
Ayatullah Haj Hussein Khadimi alizaliwa mjini Isfahani, Iran mwaka 1280 Hijiria Shamsia. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi na ya kati alielekea mjini Najaf, Iraq na kusoma kwa maulama wakubwa wa zama hizo kama vile Ayatullah Mirza Naini, Sayyid Abul-Hassan Isfahani na Sheikh Muhammad Jawad Balaghi.
Akiwa na umri wa miaka 26 alifikia daraja ya ijtihadi ambapo baada ya kurejea mjini Isfahani alijikita na shughuli ya ufundishaji sheria za Kiislamu (fiqhi) na usulu fiqhi ambapo alikuwa na wanafunzi wengi.
Katika tukio la amri ya mtawala wa wakati huo wa Iran ya kuwataka wanawake kutovaa hijabu Ayatullah Haj Agha Hussein Khadimi alitoa hotuba kali ya kupambana na utawala wa Reza Shah Pahlavi kama ambavyo pia alishiriki katika harakati mbalimbali za kupambana na njama za mkoloni Mwingereza kwa ajili ya kupora raslimali za Iran.
Siku kama ya leo miaka 14 iliyopita yaani mwaka 2004, kufuatia miripuko 5 ya mabomu kwenye vituo kadhaa vya treni ya chini ya ardhi (Metro) mjini Madrid Uhispania, watu karibu 200 waliuliwa na wengine 1000 kujeruhiwa. Miripuko hiyo inahesabiwa kuwa miongoni mwa vitendo vikubwa vya kigaidi kuwahi kutokea Uhispania na Ulaya tangu mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia.
Baada ya kutokea miripuko hiyo serikali ya wakati huo nchini humo ililituhumu kundi la Eta Basque ambalo linadai kujitenga na utawala wa nchi hiyo, kwamba ndilo lililohusika na miripuko hiyo, hata hivyo kundi la Al Qaida lilitangaza kuhusika na miripuko hiyo.
Miripuko hiyo ya Machi 11 ilitokea wakati chama cha Socialist kikiwa kimeshinda katika uchaguzi wa Bunge nchini humo na kuondoka vikosi vya Uhispania nchini Iraq.
Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita, sawa na tarehe 11 Machi mwaka 2006 dikteta wa zamani wa Yugoslavia Slobodan Milosevic akiwa na umri wa miaka 64 alifariki dunia ndani ya jela katika mji wa the Hague.
Miezi 9 baada ya kuanguka utawala wake mwaka 2001, Milosevic alitiwa mbaroni na kukabidhiwa na Yugoslavia ya zamani, kwa mahakama ya uhalifu wa kivita ya mjini the Hague.
Akiwa kijana alijiunga na chama cha Ukomonist cha Yugoslavia ya zamani.
Mwaka 1989 Milosevic akawa Rais wa Serbia. Aliongoza vita vilivyoanza mwaka 1992 vilivyo dumu kwa muda wa miaka mitatu na nusu.
Katika vita hivyo Waislamu wa Bosnia laki mbili waliuawa, huku wengine milioni 2 wakibakia kuwa wakimbizi.
Kufuatia kushindwa Milosevic katika uchaguzi wa mwaka 2000 na kushadidi upinzani wa ndani dhidi yake, hatimaye utawala wake ulianguka na baada ya muda mfupi akatiwa mbaroni. Kesi ya Milosevic ilianza kusikilizwa mwaka 2002, hata hivyo kifo chake kilitokea kabla ya kumalizika kesi hiyo.
Na siku kama ya leo miaka 7 uliyopita yaani Machi 11 mwaka 2011, tetemeko la ardhi lililokuwa na ukubwa wa daraja 9 kwa kipimo cha rishta lililikumba eneo la Tohoku lililopo mkoa wa Miyagi Mashariki mwa Japan.
Tetemeko hilo lilipelekea kuuawa watu elfu 12 na malaki ya wengine kubakia bila makazi kufuatia tetemeko hilo ambalo lilikuwa halijawahi kutokea mfano wake nchini humo kwa makumi ya miaka.
Tetemeko hilo lilibomoa miundombinu, makazi ya raia na taasisi mbalimbali na kuiletea hasara ya mabilioni ya pesa nchi hiyo, kiasi kwamba kwa muda fulani, Japan ilikuwa katika hali mbaya ya kiuchumi.
Tetemeko hilo lilizua mawimbi ya Tsunami yaliyokuwa na mwinuko wa mita 15, huku mawimbi mengine madogo madogo yakizikumba nchi nyingine za jirani kufuatia tetemeko hilo.
Comments