
Akitangaza uamuzi huo mapema siku ya Jumapili, Machi 4, 2018, mwenyekiti wa CUF wilaya ya Ubungo, ndugu Bashir Ally Muya,
amesema kuwa wamefikia uamuzi huo kutokana na Mtatiro kukaidi agizo la
chama hicho lililomtaka kujibu tuhuma mbalimbali zinazomkabili, mbele ya
Baraza la Utendaji la Wilaya ya Ubungo.
Muya amedai kuwa, mnamo tarehe 20 Desemba 2017, kamati ya utendaji ya
chama hicho ilimtaka ndugu Mtatiro, na wenzake sita kuja mbele ya
kamati hiyo kujibu tuhuma mbalimbali zinazowakabili, agizo ambalo
Mtatiro na wenzake walikaidi.
Ametaja makosa mawili makuu yaliyomfukuzisha uanachama Mtatiro kuwa
ni: kutolipia kadi yake ya uanachama kwa muda wa miaka mitatu sasa,
kitendo ambacho ni kinyume na katiba ya cha hicho, ambapo inasema endapo
mwanachama hatalipia kadi yake ya uanachama kwa muda wa mwaka mmoja
pekee, basi mwanachama huyo uanachama wake utasitishwa mara moja.
Ametaja kosa la pili kuwa ni kukihujumu (kukisaliti) chama kwa
kushirikiana na Chadema katika chaguzi za marudio zilizofanyika ndani ya
wilaya ya Ubungo, ambapo amesema licha ya chama hicho kusimamisha
wagombea, Mtatiro na wenzake hawakuwaunga mkono, huku wakitumia muda wao
mwingi kuzungumzia masuala ya Chadema.
Aidha, Muya amesema kuwa kwakuwa Mtatiro ni mjumbe wa mkutano mkuu wa
taifa, uongozi wa wilaya utamwandikia barua katibu mkuu wa CUF
kumtaarifu juu ya uamuzi huo, ili baadaye aandikiwe barua kutaarifiwa
juu ya kufutwa kwake uanachama.
Wengine waliofutwa uanachama ni: Twaha Rashidi, Mwinyi Hamis, Khalid Singano, Jumanne Athuman, Kassim Hamis, na Yusuf Lema.
Miongoni mwa sababu zilizotajwa kuwafuta uanachama ni pamoja na; kuwa
na kadi za chama cha Chadema, kumnadi mgombea wa udiwani Kata ya
Saranga kwa tiketi ya Chadema kwenye uchaguzi mdogo uliopita ilihali
chama hicho kilikuwa na mgombea, pamoja na kumkashifu mwenyekiti wa CUF
taifa kwenye mitandao ya kijamii.
chanzo: zanzibar24.
Comments