Serikali
ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo (JICA), imeipatia Tanzania
ruzuku ya Yen bilioni 3.78 sawa na Shilingi bilioni 77.3 kwa ajili ya
upanuzi wa barabara ya New Bagamoyo, kuanzia Morocco hadi Mwenge, Jijini
Dar es Salaam.
Makubaliano
ya msaada huo yametiwa saini Februari 28, 2018, Jijini Dar es Salaam na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James, kwa niaba ya
Serikali, na Balozi wa Japan nchini Tanzania Masaharu Yoshida na
kushuhudiwa na Mwakilishi Mkazi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Japani
(JICA), Toshio Nagase na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara
nchini-Tanroads, Mhandisi Patrick Mfugale.
Mradi
wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 4.3 utahusisha barabara yenye
njia nne pamoja na kuanza kwa awamu ya nne ya ujenzi wa barabara
itakayotumiwa na mabasi ya mwendo wa haraka (BRT phase IV).
Akizungumza
baada ya kutiwa saini wa makubaliano hayo, Bw. Doto James amesema kuwa
barabara hiyo ikikamilika itasaidia kutatua changamoto ya msongamano wa
magari yanayotoka na kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
“Upanuzi
wa Barabara ya New Bagamoyo si tu kwamba utaondoa msongamano wa magari,
bali pia ni kiungo muhimu cha Bandari ya Bagamoyo ambayo itarahisisha
usafirishaji wa abiria, mizigo na huduma kutoka Jiji la Dar es Salaam,
mkoa wa Pwani na mikoa mingine nchini” Alisema Bw. Doto James.
Ameishukuru
Japan kwa msaada mwingine uliotolewa mwezi Septemba, 2017 wa kiasi cha
fedha za Japan (Yen) milioni 69 sawa na shilingi bilioni 1.4 ambazo
zimetumika kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa barabara hiyo
itakayoanza kujengwa
Bw.
James ameeleza kuwa awamu ya kwanza, Japan ilitoa kiasi cha shilingi
bilioni 99.5. kujenga barabara ya njia nne katika kipande cha kilometa
12.9 kutoka makutano ya barabara ya Tegeta na makutano ya barabara ya
Mwenge pamoja na kukamilisha ujenzi wa madaraja ya Mlalakuwa, Lugalo na
Tegeta.
“Si
mara ya kwanza kwa Japan kuisaidia Tanzania, wanajenga barabara za juu
katika makutano ya Tazara, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami
kutoka Dodoma hadi Babati mkoani Manyara (km 188.15), Tunduru-Mangaka –
Mtambaswala (km 202) na barabara ya Iringa hadi Dodoma (259.9)”
alisisitiza Bw. Doto James.
Balozi
wa Japan, Mhe. Masaharu Yoshida ameeleza kuwa kutolewa kwa msada huo
ili kuwezesha awamu ya pili ya ujenzi wa barabara kuanza kutayafanya
matokeo ya kujenga barabara hiyo kuanza kuonekana dhahiri ikiwemo
kupunguza msongamano wa magari kwa kiasi kikubwa ili kuokoa fedha nyingi
zinazotokana na changamoto za msongamano huo.
“Ili
kukamilisha usanifu wa kina wa mradi huu, nilisaini mkataba wa usanifu
wa kina wa mradi wa upanuzi wa barabara ya new Bagamoyo (Awamu ya Pili)
miezi mitano iliyopita, hatimaye sasa ninasaini mkataba wa sehemu kuu
ambayo ni ujenzi wenyewe” Alisema Balozi Yoshida.
Balozi
huyo wa Japan hapa nchini, amesema mradi huo utasaidia kuboresha ukuaji
wa uchumi na kupunguza umasikini nchini na kwamba msaada huo ni
mwendelezo wa kudumisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Japan na Tanzania.
Utafiti
uliofanyika hivi karibuni unaonesha kuwa Barabara ya Bagamoyo ndiyo
yenye msongamano mkubwa wa magari yanayokadiriwa 52,000 yanayopita kila
siku katika barabara hiyo.
chanzo:Mpekuzi.
Comments