WATU
sita walifariki dunia jana na wengine sita kujeruhiwa baada ya lori la
kokoto walilokuwa wakisafiria kufeli breki na kugongana na gari la taka
la Manispaa ya Dodoma, katika gema la Mlima Ntyuka.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alithibitisha kutokea kwa ajali
hiyo na kwamba ilikuwa majira ya saa tisa alasiri.
Alisema ajali hiyo, imehusisha magari mawili ambapo moja ni lori la kokoto lenye namba T236 DHF na la taka la Manispaa.
Akizungumza
kuhusu ajali hiyo, mmoja wa mashuhuda ambaye hakupenda jina lake
liandikwe alisema lori hilo la kokoto lilipinduka katika mlima huo
likiwa limebeba abiria ambao ni wapakia kokoto.
"Hili
gari lilikuwa na abiria zaidi ya 10 ambao ni wapakiaji kokoto na
lilikuwa likiendeshwa na Baraka Malata ambaye yupo mahututi kwa sasa,"
alisema shuhuda huyo. "Huyu Baraka huwa ni utingo wa hilo lori, dereva
mwenyewe hakuwepo leo."
Alisema
lori hilo lilikuwa likishuka na kokoto kutoka kwenye mlima huo na
kwamba breki zake zilifeli na kugongana uso kwa uso na gari la taka
ambalo lilikuwa likipandisha.
Mganga
mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Dodoma, Dk. Caroline Damian
alithibitisha kupokea miili sita ya watu waliofariki na kwamba baadhi ya
majeruhi wapo katika hospitali hiyo na wengine Hospitali ya DCMC.
chanzo:Mpekuzi.
Comments