Baada ya Erdoğan kutishia kuishambulia Iraq, jeshi la Uturuki lashambulia ngome za PKK.

Baada ya Erdoğan kutishia kuishambulia Iraq, jeshi la Uturuki lashambulia ngome za PKKJeshi la Uturuki limefanya mashambuli ya anga katika maeneo yanayodaiwa na Ankara kuwa ni maficho na ngome za wapiganaji wa Kikurdi wa PKK kaskazini mwa nchi jirani ya Iraq.

Jumatano ya jana jeshi la Uturuki lilitoa taarifa likisema kuwa, operesheni za usiku wa Jumanne zilizofanywa katika maeneo ya wapiganaji hao wa PKK kaskazini mwa Iraq, zimepelekea kuuawa watu 38 miongoni mwa wapiganaji hao, sambamba na makumi ya wengine kujeruhiwa. 
Inaelezwa kuwa katika operesheni hizo, jumla ya maficho 12 ya wapiganaji hao wa Kikurdi yamesambaratishwa pamoja na kuharibiwa pia zana zao za kijeshi.
Operesheni hizo za jeshi la Uturuki zimefanyika katika hali ambayo, serikali ya Iraq inapinga vikali hatua hiyo ya Uturuki ya kufanya mashambulizi ndani ya ardhi yake bila ridhaa ya serikali ya Baghdad. 
Kufuatia hali hiyo serikali ya Baghdad imewasilisha malalamiko yake kwa Ankara juu ya operesheni hizo zinazofanywa ndani ya ardhi ya Iraq kwa kisingizio cha kuwatafuta wapiganaji wa Kikurdi wa PKK ambao wanatajwa na Uturuki kuwa ni magaidi. 
Kabla ya hapo Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki alitishia kwamba, ikiwa serikali ya Iraq haitoshirikiana na nchi yake, basi Ankara itaanzisha mashambulizi katika miji ya Sinjar nchini Iraq dhidi ya wanachama wa kundi hilo la Kikurdi la PKK.
Hayo yanajiri katika hali ambayo Uturuki pia, ilianzisha mashambulizi ya kijeshi nchini Syria kwa kizingizio kama hicho cha kuwatafuta wapiganaji wa Kikurdi ambao inawataja kuwa ni magaidi na hadi sasa jeshi la Uturuki limetia kambi mjini Afrin, kaskazini mwa Syria baada ya kuushibiti mji huo, huku likiwa halijaeleza iwapo litaondoka kutoka mji huo hivi karibuni. 
Mchakato wa kutatuliwa tatizo la Wakurdi nchini Uturuki, ulianza mwezi Disemba mwaka 2012, hata hivyo mchakato huo ulisimama baada ya kutokea mripuko wa mwaka 2015 mjini Suruç Uturuki. 
Kuanzia wakati huo, jeshi la Uturuki lilianzisha mashambulizi makali dhidi ya wanachama wa kundi hilo.
chanzo:parstoday.

Comments