Zarif: Sera za nyuklia za Trump zinalenga kuangamiza wanadamu.

Zarif: Sera za nyuklia za Trump zinalenga kuangamiza wanadamuWaziri wa Mambo ya nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali sera mpya za nyuklia zilizotangazwa na utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani na kusema zinalenga kuangamiza wanadamu wote duniani.

Katika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Twitter, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema: "Sera za nyuklia za Marekani zinaonyesha namna nchi hiyo inavyotegemea silaha za nyuklia jambo ambalo ni ukiukwaji wa mkataba wa kimataifa wa NPT wa kuzuia uundwaji na usambazwaji wa silaha za nyuklia." 
Zarif amesema silaha hizo za Marekani zimepelekea jamii ya mwanadamu ikaribie zaidi katika nukta ya kuangamizwa kikamilifu. 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema tokea Marekani itumie silaha za nyuklia mwaka 1953 sasa dunia inakumbwa tena na hatari ya utumizi wa silaha za nyuklia. 
Aidha amesema azma ya Trump ya kuvuruga mapatano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji JCPOA ni mfano wa wazi wa sera hizo hatari za Trump.
Siku ya Ijumaa Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, ilitangaza sera mpya za nyuklia katika fremu ya 'Tathmini ya Hali ya Nyuklia-NPR.' Kwa mujibu wa sera hii mpya ya kistratijia, utawala wa Trump utaendeleza sehemu kubwa ya sera za nyukli za Marekani zilizotumika wakati wa utawala uliotangulia wa Barack Obama sambamba na kuchukua msimamo mkali na wenye uhasama zaidi kuhusu Russia. 
Aidha utawala wa Trump unasisitiza kuimarisha zaidi maghala ya silaha za nyuklia za Marekani.
chanzo:parstoday.

Comments