Yawanunulia viatu.


YANGA wajanja sana. Kwa kutambua kuwa wanahitaji nguvu kubwa ili kushinda mechi yao ya marudiano dhidi ya St. Louis ya Shelisheli, wameamua kuweka mpango wa haraka ukiwamo kumtanguliza kiongozi mmoja huko aliyekwishaanza kuandaa mazingira ya ushindi.
Ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya St. Louis katika mechi ya kwanza ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, unaifanya Yanga kuuingia mchezo wa Jumatano ijayo kwa tahadhari kubwa, hivyo kuamua kumtanguliza mtu.
Kwa Mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hussein Nyika, aliyetangulizwa Shelisheli ni Katibu wa kamati hiyo, Samuel Lukumay, ambaye tayari ameshaanza kutoa taarifa zitakazowasaidia kupata ushindi katika mchezo huo.
Lukumay ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Yanga, tayari amebaini mambo kadhaa huko, lakini kubwa ambalo ameudokeza uongozi wa timu hiyo ni kwamba wanahitaji viatu maalumu vya kucheza kwenye matope kwani wapinzani wao wanapenda kulowesha sana uwanja hata kama hakuna mvua.
Nyika alisema Lukumay amewaambia kwamba kitu cha kwanza wanachotakiwa ni kuwanunulia wachezaji wote watakaosafiri viatu vyenye uwezo wa kutumika katika uwanja huo, jambo ambalo tayari wameanza kulifanyia kazi.
Alisema mmoja wa viungo wa Kitanzania anayecheza ligi ya huko, pia amewaambia kuwa St. Louis si timu ngumu, lakini sasa wameanza kukomaa na kujua fitna za kumwagia uwanja wao maji ambapo Yanga inahitaji kuwa na viatu hivyo kujiweka sawa na hilo.
Mbali ya hilo, Nyika alisema Lukumay amekuwa katika wakati mgumu kutafuta hoteli na uwanja wa mazoezi ambao timu yao itautumia kwani kocha wao, George Lwandamina, ameelekeza hivyo vyote visiwe mbali na uwanja wa mchezo ili safari zisiwachoshe wachezaji.
“Tumeshaanza kujipanga tayari kwa mchezo huo, hivi tunavyoongea nipo njiani tunakwenda kufanyia kazi mambo ambayo mwenzetu aliyetangulia ameanza kutupa taarifa za msingi.
“Kubwa tumetakiwa kununua viatu vinavyohimili uwanja uliomwagiwa maji mengi,” alisema Nyika.
“Ametuambia kwamba hizo ndiyo mbinu za hao jamaa na si kwamba ni timu ngumu, lakini wana mambo mengi ya fitna za mchezo uwanjani na vyumbani, pia ametuambia kuna joto kali hili la hapa Dar es Salaam tunaloumia nalo kule ni mara mbili, kwa hiyo ni vyema timu ikawahi ili izoee.”
MIPANGO IKO HIVI
Akizungumzia maandalizi ya kiufundi, Nyika alisema amekuwa akihudhuria mazoezi ya siku tatu sasa na kocha wao amekuwa akisisitiza wachezaji kujaribu kupiga mashuti makali na kwamba mabao yao mawili yaliyofungwa juzi na viungo Emmanuel Martin na Papy Kabamba Tshishimbi dhidi ya Majimaji ni matunda ya maandalizi hayo.
“Wakati uongozi tunajiandaa na hayo, naridhishwa na maandalizi ambayo makocha wetu wamekuwa wakiyafanya,” aliongeza Nyika.
“Wanayanga wanafurahia mabao ya mashuti mawili tuliyofunga jana (juzi) lakini nikwambie hiyo ni mipango ya kocha, amekuwa akitaka mashuti ya mbali yenye nguvu na yanayolenga lango,” alisema Nyika.”
chanzo:Mwanasport.

Comments