Yanga yaweka rekodi, yaitajirisha Lipuli FC.

LICHA ya kipigo, lakini klabu ya Lipuli FC imenufaika na ujio wa Yanga mjini hapa baada ya kuvuna kiasi cha Sh18 milioni kutokana na mgao wa mapato ya pambano lao la Ligi Kuu Bara lililopigwa juzi Jumamosi ambapo liliingiza Sh 58.4 milioni.
Kiwango hicho cha fedha ni rekodi kwa Uwanja wa Samora, kwani haijawahi kutokea pambano lolote, sio la msimu huu tu bali hata mechi za nyuma kuingiza kiasi kama hicho cha fedha.
Yanga ilioibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye mchezo huo, iliambulia Sh 9 milioni na msimamizi wa kituo hicho, Elias Mwanjala alisema katika makusanyo hayo mbali na fedha zilizopata Lipuli na Yanga fedha nyingine zilipelekwa kwenye maeneo mengine kama  gharama za mchezo, kodi, TFF na Bodi ya Ligi.
“Hii  imevunja rekodi katika Uwanja wa Samora kwani umeingiza Sh 58.4 milioni, haijawahi tokea kabisa na katika mchezo ule hakuna hata tiketi moja iliyobainika kuchachukuliwa. Kulikuwa na usimamizi mzuri sana kwenye suala la tiketi,” alisema.
Mwanjala alisema katika makisio yao ilikuwa waingizie mashabiki 10,000 uwanjani lakini hali ilikuwa tofauti, watu walizidi mara madufu.
Akizungumzia hatua ya timu zote mbili kugoma kuingilia geti kuu na badala yake kuamua kutumia geti dogo linalotumiwa na viongozi, Mwanjala alisema timu zote zilivunja kanuni za mpira na adhabu yake ni kupigwa faini.


“Unajua klabu hizi zinaamini katika ushirikina, kitu ambacho TFF hatuamini katika jambo hilo,  hivyo wanaona bora walipe faini na hata suala la wachezaji kutoingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo ni kosa ambalo pia linastahiki kupigwa faini, kwa kuwa ni kosa kufanya hivyo.”

Comments