VIJANA wa Jangwani, Yanga, tayari wapo ugenini Shelisheli wakijiandaa kuwavaa wenyeji wao, St. Louis wanaorudiana nao katika mechi ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku wakianza kuhesabu saa 288 ngumu na za hatari kwao.
Hata hivyo, benchi la ufundi la klabu hiyo chini ya Mzambia George Lwandamina, limepiga hesabu zake na kuamini kama watavuka salama ndani ya saa hizo ambazo ni sawa na siku 12, kila kitu kwao kitakuwa freshi na mashabiki wao lazima watabasamu.
Kocha Lwandamina na wenzake wameiangalia ratiba inayowakabili kuanza mechi yao ya keshokutwa Jumatano huko Shelisheli na kujikuta wakishtuka, lakini wakatiana moyo kwamba huo ndio wakati wa kukomaa ili wavuke na kupeta kiulaini.
Ipo hivi; Yanga inakabiliwa na mechi ngumu nne zinazoihitaji kupambana kwelikweli ili kuukwepa mtego waliowekewa kwa sasa na kama ikatokea wakateleza, basi lazima ile kwao na kuwapa kicheko watani zao wa Simba wanaowafuatilia.
Yanga inashuka uwanjani keshokutwa kumalizana na St. Louis, lakini mara baada ya mchezo huo kikosi hicho kinatakiwa kiombe kisikumbane na aibu ya kuchelewa ndege kama ilivyotokea msimu uliopita nchini Algeria, kwani kinatakiwa kupanda ndege fasta na kurejea jijini Dar es Salaam kuwahi mechi nyingine ugenini.
Ndio, baada ya mchezo huo wa Shelisheli ambao Yanga inahitaji sare tu kuvuka ili kuingia raundi ya kwanza, itatakiwa kurejea jijini Dar es Salaam na kwa vyovyote vile kama hawatakuwa na fedha wanatakiwa kuanza safari kuelekea mjini Songea kwa ajili mchezo wao wa Raundi ya Tatu ya Kombe la FA dhidi ya Majimaji.
Mchezo huo umepangwa kupigwa Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Majimaji na lazima mshindi apatikane kwa ajili ya kuingia robo fainali ya michuano hiyo na kwa bahati mbaya ni kwamba rekodi ya vijana wa Jangwani mkoani Ruvuma haivutii.
Achana na rekodi mbovu mjini Songea, Yanga baada ya mchezo huo itatakiwa tena kufunga safari mpaka mjini Mtwara kwa ajili ya kuvaana na wenyeji wao Ndanda FC katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa Februari 28 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.
Kama ulidhani vijana wa Lwandamina watakuwa wamepumua baada ya kufanya safari hizo za kuunga, pole yako, kwani itatatakiwa kufanya safari nyingine hadi mjini Morogoro ili kuwakabili Wakata Miwa wa Manungu, Mtibwa Sugar.
Mechi hiyo itapigwa Machi 4, siku chache kabla ya kuanza pilikapilika za maandalizi ya mchezo wao wa mkondo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana ama El Merreikh ya Sudan, lakini kama watavuka salama mbele ya Washelisheli.
MSIKIE KOCHA
Ugumu wa ratiba hiyo umemshtua Lwandamina anayewategemea nyota wake wakiongozwa na Papy Kabamba Tshishimbi, Ibrahim Ajibu na wengine kufanya kweli ameliambia Mwanaspoti kuwa mpaka sasa hajajua ni nani aliyepanga ratiba hiyo inayompa kazi ya kupiga hesabu kali ili kukwepa matokeo mabaya.
Lwandamina alisema mechi zote nne zimekaa karibu sana ikiwa ni ndani ya siku 12 akitakiwa kuomba wasikumbane na matokeo mabaya, pia kukwepa kupata majeruhi zaidi katika kila mchezo, vinginevyo wanaweza kuteleza na kuwapa faida wapinzani wao.
“Hii ni moja kati ya ratiba ngumu tuliyonayo sijajua waliopanga walizingatia nini kwa sababu haiipi timu afya ya maandalizi mazuri, hizi timu zinazoshiriki mashindano ya CAF ratiba zake zilitakiwa kuzingatia jiografia ya safari wanazotakiwa kufanya katika mchezo mmoja kwenda nyingine,” alisema Lwandamina.
“Inawezekana ni bora pale mtakapokuwa mnatumia usafiri wa ndege, lakini kuna safari za hapa ndani ndege hazitumiki mnalazimika kusafiri kwa barabara wachezaji wanachoka sana, nafikiri tunatakiwa kujipanga vyema katika ratiba ya namna hii, imenishtua sana.”
chanzo:Mwanansport.
Comments