Yakubu: Okwi? Namsubiri tu.

BEKI, Yakubu Mohammed wa Azam FC, amesema licha ya straika wa Simba, Emmanuel Okwi, kuongoza kwa mabao katika Ligi Kuu Bara, lakini hana hofu naye watakapokutana keshokutwa Jumatano kwenye mechi yao ya marudiano ya Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na Mwanaspoti, Yakubu, alisema anatambua Okwi ni mfungaji mzuri, lakini hilo halimtishi na badala yake anamkaribisha katika mechi yao ili watu wapate majibu yeye ni beki wa aina gani na Azam ni timu ya daraja lipi.
“Mshambuliaji yeyote ninayekutana naye huwa nacheza kwa umakini wa hali ya juu kuhakikisha kwamba hawezi kuleta madhara katika lango letu, hata Okwi sina maneno mengi ila nataka tukutane uwanjani ndiko  kwenye majibu kamili,” alisema.
Yakub aliongeza watu wengi wamekuwa wakiongelea mechi hiyo kwamba Okwi anaweza akaifunga Azam, huku wakisahau kwamba Azam yenyewe pia ina straika Bernard Arthur ambaye naye ni balaa kwa kutupia kambani.
Okwi alishindwa kumalizia mchezo wao wa jana Jumapili dhidi ya Ruvu Shooting baada ya kuumizwa kooni na beki Mau Boffu aliyelimwa kadi nyekundu kwa kosa hilo.


Yakubu akizungumzia zaidi kuhusu presha ya mchezo huo alisema, presha haiwezi kukimbilika kutokana na aina ya mechi na timu ambayo unakutana nayo, badala yake inabidi utilize presha na kufanya kazi vizuri bila kuwa na presha yoyote.

Comments