Waziri Mkuu Atembelea Kiwanda Cha Nyama Misungwi.....Kina Uwezo Wa Kuchinja Ng’ombe 600 na kondoo 900 Kwa Siku.
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametembelea na kukagua kiwanda cha kusindika nyama
cha Kampuni ya Chobo Investment kilichpo wilayani Misungwi chenye uwezo
wa kuchinja ng’ombe 600 mbuzi na kondoo 920 kwa siku.
Alitembelea
kiwanda hicho kinachomilikiwa na wazawa jana (Jumatatu, Februari 19,
2018) wakati akiwa katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi mkoani
Mwanza. Alisema amefarijika na uwekezaji huo.
Alisema
uwekezaji wa aina hiyo ulikuwa unasubiriwa sana nchini kwa sababu
unakwenda kupunguza tatizo la wafugaji kutokuwa na soko la uhakika wa
mifugo yao, hivyo Serikali itamuunga mkono ili kiwanda hicho kiwe
endelevu.
Waziri
Mkuu alisema Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza sera ya uchumi wa
viwanda na inahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika
viwanda mbalimbali, ambapo aliipongeza kampuni hiyo kwa kuunga mkono
jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kukuza uchumi kupitia sekta ya
viwanda
Akizungumzia
kuhusu changamoto ya kutokuwa na maeneo ya kunenepeshea na kulisha
mifugo yao, Waziri Mkuu alisema tayari alishamuagiza Waziri wa Mifugo
Bw. Luhaga Mpina kushughulikia suala hilo na kwamba litapatiwa ufumbuzi.
Pia Waziri Mkuu aliwataka watumishi waliojiriwa katika kiwanda hicho wafanye kazi kwa bidii, wawe waaminifu na waadilifu.
Awali,
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Bw. John Chobo alisema kiwanda hicho
kinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji, hivyo
kinategemea maji ya kisima au ya kuletwa na boza kutoka Mwanza mjini
jambo ambalo linachangia katika kuongeza gharama za uzalishaji.
Baada
ya kutoa malalamiko hayo Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa MWAUWASA,
Mhandisi Anthony Sanga kushughulikia suala hilo na ahakikishe kiwanda
hicho kinapata maji. Kiwanda hicho kipo umbali wa kilomita nne kutoka
Ziwa Victoria.
Akizungumzia
kuhusu changamoto ya eneo la kulishia na kunenepeshea ng’ombe Bw. Chobo
alisema kampuni yake iliomba kupatiwa eneo kutoka kwa Serikali tangu
mwaka 2014 karibu na kiwanda hicho lakini hadi sasa hawajapatiwa.
Kiwanda
hicho kinauza bidhaa zake ndani na nje ya nchi. Nchi hizo ni Oman,
China, Canada na Misri. Baadhi ya wanunuzi hao kutoka Omani ni Bw. Tahir
Al Hashim na kutoka China ni Bw. Kingsong Shao walisema nyama
inayochakatwa kiwandani hapo ni nzuri na ina ubora wa kimataifa.
Pia
kiwanda hicho kinasambaza nyama katika migodi yote mikubwa nchini
ambayo awali ilikuwa inaagiza nyama kutoka nje ya nchi, hivyo,
Mkurugenzi wa kiwanda hicho aliiomba Serikali kuwasaidia katika kulinda
soko la ndani.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, FEBRUARI 20, 2018
chanzo:Mpekuzi.
Comments