Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na
Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta wamewaagiza Mawaziri
wa Tanzania na Kenya kutatua tofauti ndogondogo zinazojitokeza katika
biashara kati ya nchi hizi mbili.
Marais
hao wametoa maagizo hayo leo asubuhi tarehe 23 Februari, 2018
walipokutana na kufanya mazungumzo katika hoteli ya Munyonyo mjini
Kampala muda mfupi kabla ya kuanza kwa vikao vya mkutano wa wakuu wa
nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mhe.
Rais Magufuli na Mhe. Rais Kenyatta wamesema wanataka kuona biashara
kati ya Tanzania na Kenya inazidi kukua na bidhaa zinauzwa na kununuliwa
baina ya nchi hizo bila vikwazo vyovyote na hivyo kuagiza tofauti
zilizojitokeza katika baadhi ya bidhaa zimalizwe.
“Kuna
mambo madogomadogo yanakuwa yanajitokeza katika biashara kati ya Kenya
na Tanzania, tunataka kwa haya yote Mawaziri wa Kenya na Mawaziri wa
Tanzania mkae myatatue, sisi hatuna tatizo, mambo mengine madogomadogo
mno, mambo ya viatu, nguo, ngano, gesi ni madogo sana, mnatakiwa
myatatue nyinyi yasifike kwetu, sisi huku tuko sawasawa” amesema Mhe.
Rais Magufuli na kuungwa mkono na Mhe. Rais Kenyatta.
Wametoa
maagizo hayo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki wa Tanzania Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria
wa Tanzania Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya
Balozi Monica Juma na Waziri wa Afrika Mashariki na Maendeleo ya
Ushoroba wa Kaskazini wa Kenya Mhe. Peter Munya.
Wakati
huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa
Jamhuri ya Sudani Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit katika hoteli ya
Munyonyo Mjini Kampala.
Baada
ya Mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania kama ilivyo kwa
nchi nyingine za Afrika Mashariki inaguswa na hali ya Sudani kusini na
ametoa wito kwa pande zinazopingana kumaliza tofauti zao ili wananchi wa
Sudani Kusini wajikite kujenga nchi yao.
“Nimemhakikishia
Mhe. Rais Salva Kiir kuwa Tanzania ipo pamoja na Sudani Kusini na
tunapenda tofauti zinazosababisha matatizo nchini mwake ziishe, sisi
Tanzania tupo tayari kufanya biashara na Sudani Kusini, hata chakula
kama wanahitaji tutawauzia” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Salva Kiir Mayardit amesema Tanzania na Sudani
Kusini zina uhusiano wa kihistoria tangu enzi ya Baba wa Taifa Hayati
Mwl. Julius Kambarage Nyerere na kwamba japo kuna vita nchini mwake Mhe.
Rais Magufuli amemhakikishia kuwa uhusiano na ushirikiano huo
utaendelezwa na kukuzwa zaidi.
Katika
hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Gaston Sindimwo.
Mhe.
Gaston Sindimwo amemfikishia ujumbe wa Rais wa Burundi Mhe. Pierre
Nkurunziza kuwa hali ya Burundi ni shwari na Mhe. Rais Magufuli amesema
anafurahi kuona sasa wakimbizi wa Burundi waliokuwa wamepata hifadhi
Tanzania wameanza kurudi nchi kwao.
Mhe.
Rais Magufuli pia amefanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu
wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa ambaye ni mratibu wa mazungumzo
ya amani ya mgogoro wa Burundi aliyealikwa kuhudhuria mkutano wa 19 wa
wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hapa Kampala.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kampala
23 Februari, 2018.
chanzo:Mpekuzi.
Comments