VIDEO-Chadema yaishukia NEC kubadili vituo 46 vya kupigia kura.


Image result for chadema
Wakati kampeni za uchaguzi zikiendelea, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeridhia kuhamishwa vituo 46 vya kupigia kura katika kata tatu za Jimbo la Kinondoni hatua ambayo imepingwa vikali na Chadema ikisema vyama havikushirikishwa katika uamuzi huo.
Uchaguzi mdogo katika jimbo hilo na la Siha pamoja na kata 10 utafanyika Februari 17.
Hata hivyo, katika taarifa yake aliyoitoa jana, Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima amesema uamuzi wa NEC kuridhia kuhamishwa kwa vituo hivyo, umetokana na makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Kinondoni na vyama vya siasa.
Alisema vituo hivyo ni vilivyokuwa kwenye nyumba za ibada, zahanati na maeneo ya majengo ya watu binafsi.
Lakini mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano, uenezi na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema alisema chama chake hakikushirikishwa na hivyo kinalaani uamuzi huo.
Mrema alisema hakuna uandikishaji mpya wa wapigakura uliofanyika hivyo uhamishaji wa vituo hauna nia njema.
Alisema katika kampeni, walishawaeleza wananchi kuwa watapiga kura katika vituo walivyotumia mwaka 2015 na kuhoji watarudi vipi kuwaeleza kuwa vimebadilishwa.
Alisema katika uchaguzi mdogo wa udiwani kwa kata 43 uliofanyika Novemba 26 mwaka jana, baadhi ya vituo vilihamishiwa karibu na vituo vya polisi.
Katika taarifa yake, NEC inasema imeridhika na uamuzi huo kwa sababu hatua zilizochukuliwa ni sahihi kwa mujibu sheria.
“Tumejiridhisha kuwa baadhi ya vituo katika Kata ya Kigogo vilikuwa katika nyumba za ibada na vingine kuwa katika maeneo yenye ufinyu wa nafasi hivyo tumeridhia vituo hivyo vihamishwe na kupelekwa katika majengo ya umma,” alisema Kailima.
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Mwananyamala , Barima Omari alisema vituo vinane vilivyokuwa katika Shule ya Sekondari Kambangwa, Mtaa wa Msisiri A vimehamishwa na kati ya hivyo, sita vitakuwa katika ofisi ya Serikali ya Mtaa ya Msolomi na viwili katika Uwanja wa Kwakopa.
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Kijitonyama, Elizabeth Minga alisema vituo sita vilivyokuwa katika Shule ya Sekondari Kenton vimehamia Shule ya Msingi Mapambano na vitano vilivyokuwa nje ya ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Bwawani vimehamishiwa mbele ya ofisi hiyo.
Elizabeth alisema vituo sita vilivyokuwa nje ya Soko la Makumbusho vimehamia ndani ya ofisi ya meneja wa soko na vituo vitano vilivyokuwa katika ofisi ya Serikali za Mitaa Kijitonyama vimehamishiwa katika Shule ya Msingi Kijitonyama.
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Kigogo, Singoro Mdegela alisema vituo 16 vimehamishwa; vitano vilivyokuwa eneo la Kiwenge kwenye Msikiti wa Shia vimehamia Uwanja wa People na sita vilivyokuwa kwenye Zahanati ya Kigogo vimehamishiwa Shule ya Msingi Kigogo na vituo vitano katika ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mkwajuni vimehamishiwa katika Shule ya Sekondari Kigogo.
Kampeni zaendelea
Wakati mabadiliko hayo yakitangazwa, kampeni zimeendelea na jana, mgombea wa CCM Jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia alisema iwapo atachaguliwa atatoa magari ya kuzoa taka katika kata zote wilayani Kinondoni.
Akihutubia katika Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Mama Salma Kikwete, alisema atafanya hivyo kwa kuwa anajua matatizo ya wakazi wa jimbo hilo.
“Jana niliahidi kutoa Sh10 milioni kwa Saccos ya Kigogo nanyi nawaambia mkiunda mje kwa mbunge kuchukua fedha yenu ipo,” alisema.
Kuhusu gharama za kuhifadhi maiti mochwari alisema, “Hili nalituma kwa mheshimiwa Rais haliko ndani ya uwezo wangu, naomba alisikilize ningependa wananchi wa Kinondoni wahifadhi miili ya wapendwa wao hospitali bila kulipa chochote.”
Katibu wa da wa CCM aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, Katibu wa siasa na uhusiano wa kimataifa wa CCM, Ngemela Lubinga alisema, “Tumeshatenga Sh70 milioni kwa ajili ya ujenzi wa vyoo vya stendi ya Mwenge. Mchagueni Mtulia asimamie kazi zenu ikiwamo kutumia vyema fedha za Wilaya ya Kinondoni zikiwamo Sh40 milioni za ukarabati wa Shule ya Mama Salma Kikwete. “Mpeni kura Mtulia akasimamie Sh45 milioni za mikopo ya kina mama na vijana. Najua mlikuwa mnacheleweshewa, lakini kwa hili jembe sina shaka mtapata kama inavyostahili.”
Mgombea wa Chadema jimboni humo, Salum Mwalimu akizungumza katika mkutano uliofanyika Hananasif alisema, “Mkinichagua hii biashara ya kuvunja nyumba za watu bila taarifa za kutosha na fidia itakuwa mwisho, nakwenda kushughulika na hilo. Nazungumza kwa uchungu kwa kuwa naelewa matatizo ya wakazi wa Hananasif, nami nyumba yangu inaweza kubomolewa.”
Mgombea wa CUF jimboni humo, Rajab Salum akihutubia mkutano Tandale alisema endapo atachaguliwa, atawasaidia bodaboda kusajiliwa na kutambuliwa; atashawishi kuwepo mlo mmoja shuleni; motisha kwa walimu; na kuchochea kuhakikisha gharama za kuhifadhi maiti zinaondolewa
Nyongeza na Elizabeth Edward, Kalunde Jamali na Kelvin Matandiko

chanzo:Mwananchi.

Comments