Velayati: Iran ndiyo nchi yenye nguvu zaidi Mashariki ya Kati.

Velayati: Iran ndiyo nchi yenye nguvu zaidi Mashariki ya KatiMshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa amesema kuwa, Iran ndiyo nchi yenye nguvu zaidi katika eneo nyeti zaidi duniani yaani Mashariki ya Kati.

Shirika la habari la Mehr limemnukuu Dk Ali Akbar Velayati akisema hayo jana usiku katika mkutano wa wanafunzi wa vyuo vikuu wanaounga mkono Intifadha ya Palestina huko Mash'had, kaskazini mashariki mwa Iran na kuongeza kuwa: 

Kwa miaka kadhaa sasa Marekani imekuwa ikifanya njama za kuzisambaratisha nchi za eneo hili na kuunda Mashariki ya Kati Kubwa lakini imeshindwa. Amesema, matukio ya Libya, Syria, Iraq na Yemen ni sehemu ya njama hizo za Marekani.
Velayati amelaani vikali njama hizo za Marekani zenye shabaha ya kuzisambaratisha nchi za eneo hili na kusema kuwa, hata harakati mpya za hivi sasa za kijeshi za Marekani nchini Syria zinafanyika kwa lengo hilo hilo la kuzigawa nchi za Mashariki ya Kati.

Amesema, Wamarekani kamwe hawatafanikiwa katika uadui wao wa kuigawa vipande vipande Syria na kwamba imma watatoka wenyewe mashariki mwa Mto Furati au taifa la Syria litawatimua katika eneo hilo.

Vile vile amesema, Hizbullah ya Lebanon imekuwa imara sana kwa msaada wa Iran kiasi kwamba hivi sasa majenerali wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel wanakimbia kuingia vitani na Hizbullah. Amesema, hata katika vita vya Ghaza pia, Wazayuni wamekwama kutokana na muqawama wa wananchi mashujaa wa Palestina.
chanzo: parstoday.

Comments