Abdul Aleem, msemaji wa Maumoon Abdul Gayoom, rais wa zamani wa Maldives ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, rais huyo alikamatwa na maafisa wa polisi jana Jumatatu katika makazi yake, akiwa pamoja na mume wa binti yake.
Rais huyo wa zamani wa Maldives ametiwa mbaroni masaa machache baada ya rais wa sasa Abdulla Yameen kutangaza hali ya hatari nchini humo kwa siku 15.
Rais Yameen amekataa kutii agizo la Mahakama ya Juu ya nchi hiyo iliyomtaka awaachie huru viongozi wa upinzani wa kisiwa hicho cha Bahari Hindi wanaozuiliwa, akiwemo Farish Gayoom, mbunge wa upinzani ambaye pia ni mtoto wa kiume wa rais huyo wa zamani.
Ifahamike kuwa, Gayoom ni ndugu wa kambo wa Rais Yameen, na alioongoza nchi hiyo ya kusini mwa bara Asia kwa miaka 30, toka mwaka 1978 hadi 2008.
Kadhalika muda mfupi baada ya tangazo la jana la hali ya hatari, maafisa usalama walivamia jengo la Mahakama ya Juu na kuwakamata majaji wawili wa mahakama hiyo akiwemo Jaji Mkuu, Abdulla Saeed.
Rais Yameen amekuwa akikandamiza wapinzani na wakosoaji wake tangu aingie madarakani mwaka 2013.
chanzo:parstoday.
Comments