
Hayo yamesemwa huko Baraza la Wawakilishi Chukwani na Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Utawala Bora Idara za Maalum ya Baraza la Wawakilishi Mhe Machano Othman Said wakati akiwasilisha Muhtasari wa Ripoti ya Kamati hiyo kwa mwaka 2017-2018.
Alisema Kamati imeridhishwa na ukusanyaji wa mapato wa Manispaa hizo ambazo ni mpya hivyo ipo haja kwa serikali kuongeza juhudi zitakazosaidia kuleta mabadilko ya maendeleo na kuongezo kipato nchini.
“Kamati yetu kwa kiasi kikubwa imeridhishwa na ukusanyaji wa mapato wa Manispaa hizi ambazo ni mpya na tunaomba wazidi kuongeza juhudi”, alieleza Mhe Machano Othman.
Alieleza kuwa Manispaa hizo zinafanya kazi kubwa japo kuwa zinakabliwa na changamoto nyingi ikiwemo ongezeko kubwa la idadi ya wakaazi na wahamiaji kutoka maeneo tofauti.
Changamoto zingine ni ubovu wa miundombinu ya barabara, upungufu wa huduma za kijamii ikiwemo maji safi na salama, umeme na Skuli za msingi katika maeneo ya Manispaa hizo.
Aidha Mwenyekiti huyo alifahamisha kuwa, kuwepo kwa bandari zisizo rasmi katika maeneo ya Uzi na Bungi huchangia vitendo vya kihalifu ikiwemo kuvamiwa Wageni na uingizwaji wa bidhaa za magendo na zisizokuwa na Viwango vya ubora.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo alieleza kuwa mbali na changamoto zinazojitokeza katika Manispaa hizo maendeleo ya manispaa hizo yanaonekana.
Kuhusu Afisi ya Mufti, Kamati hiyo imeishauri Wizara ya Katiba na Sheria kuwapatia jenereta kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la nishati ya umeme katika Afisi hiyo.
Kamati hiyo imeishauri pia Afisi ya Mufti Zanzibar kufuatilia kiundani utendaji wa Afisi ya Mufti Pemba ili kuhakikisha kuwa wanaboresha utendaji wao katika majukumu yao ya msingi.
Wakichangia Ripoti hiyo baadhi ya Wajumbe wa Baraza hilo wamesema tatizo la rushwa bado linaendelea kuwepo na kupelekea baadhi ya kesi kukwama katika manipaa hizo.
Hivyo wameziomba taasisi husika kupambana kikamilifu na tatizo la Rushwa ambalo linaendelea kuwaathiri Wananchi wengi katika harakati za maisha yao.
chanzo:Zanzibar24.
Comments