Serikali imesema kuanzia Aprili 2018 itaanza kutoa chanjo kuwakinga wasichana kupata saratani ya mlango wa kizazi (HPV vaccine).
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema chanjo hiyo itatolewa kwa wasichana wenye umri wa miaka tisa hadi 14.
“Niwaombe wazazi na walezi wenzangu tuwe tayari kuhakikisha binti zetu wanapata chanjo hii,” amesema Ummy katika taarifa aliyoitoa leo Februari 4,2018 ikiwa ni siku ya saratani duniani.
Katika kuadhimisha siku hiyo, Ummy amehimiza kila mmoja kupima ugonjwa wa saratani ambayo amesema inatibika endapo itagunduliwa mapema.
Amesema Serikali itaendelea na jitihada za kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu vyanzo vinavyosababisha saratani ili kila mmoja aweze kujikinga.
Ummy amevitaja vyanzo hivyo kuwa ni mtindo wa kimaisha kama vile uvutaji wa sigara, ulaji wa vyakula usiofaa (kula vyakula vyenye mafuta mengi, kutokula matunda na mbogamboga za kutosha); matumizi ya pombe kupita kiasi; matumizi ya dawa za kulevya; na kutofanya mazoezi.
“Tutaongeza jitihada katika kuamsha ari na hamasa ya wananchi kupima saratani ili kujua hali zao sambamba na kusogeza huduma za uchunguzi na matibabu ya mabadiliko ya awali ya saratani katika maeneo mbalimbali na hasa vijijini,” amesema.
Waziri Ummy amesema mwaka 2017 Serikali iliongeza vituo 100 kutoka 343 vilivyopo awali kwa ajili ya huduma za kupima na matibabu ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupambana na saratani.
Amesema vituo hivyo ambavyo ni zahanati, vituo vya afya na hospitali vimepatiwa vifaa tiba na utaalamu ili kuwezesha wanawake wengi kupima saratani ya kizazi na ya matiti pamoja na kupata matibabu ya mabadiliko ya awali ya saratani ya kizazi papo hapo.
Amesema wamelenga kuwafikia wanawake milioni tatu nchi nzima ifikapo Desemba 2018.
Ummy amesema Serikali inaendelea na jitihada za kusogeza huduma za matibabu ya saratani kwa njia ya dawa (chemotherapy) na mionzi (radiotherapy) katika hospitali za rufaa za kanda (Mbeya, Bugando na KCMC).
Amesema Serikali inaendelea kuimarisha huduma za matibabu ya saratani katika Hospitali ya Ocean Road kwa kuweka mashine mbili mpya za kisasa zitakazosaidia kupunguza muda wa kusubiri kwa wagonjwa kupata huduma za tiba ya mionzi na kuhakikisha upatikanaji wa dawa kwa asilimia 100.
Waziri amesema tatizo la saratani limekuwa likiongezeka kila mwaka; Shirika la Afya Duniani (WHO) likikadiria kuwa, kila mwaka wagonjwa wapya wapatao 50,000 hugundulika na saratani za aina mbalimbali Tanzania.
Amesema kati ya hao ni wagonjwa 13,000 tu, sawa na asilimia 26 ndio wanaofika hospitali kupata matibabu.
Ummy amesema wagonjwa wengi ambao ni takriban asilimia 70 hufika hospitali kwa matibabu wakiwa katika hatua za mwisho za ugonjwa (hatua ya 3 na ya 4), hali ambayo hupunguza uwezekano wa wagonjwa kupona maradhi hayo.
Amesema takwimu za mwaka 2016/17 kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road zinaonyesha saratani zinaoongoza nchini ni ya Kizazi kwa asilimia 32.8, matiti (asilimia 12.9), Ngozi -kaposis sarcoma (asilimia 11.7), kichwa na shingo (asilimia 7.6), matezi (asilimia 5.5), damu (asilimia 4.3), kibofu cha mkojo (asilimia 3.2), ngozi -skin (asilimia 2.8), macho (asilimia 2.4), na tezi dume (asilimia 2.3).
chanzo:Mwananchi.
Comments