Minziro achana naye kabisaa.

KMC imekuwa timu ya kwanza kutoka Wilaya ya Kinondoni kucheza Ligi Kuu tangu klabu za Twiga Sports na Villa Squad kushuka daraja miaka sita iliyopita.
Klabu hiyo mpya imepanda juzi baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi la Mlale JKT na kuungana na timu za Coastal Union na JKT Ruvu zinazorejea tena katika ligi hiyo kwa msimu ujao.
Hata hivyo, kama hujui ni kwamba Kocha wa timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni, Fred Felix Minziro, ndiye mpango mzima wa klabu hiyo kucheza Ligi Kuu baada ya msimu uliopita wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kukwamia njiani.
Hata hivyo, zaidi, nyota huyo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, ameweka rekodi ya kuwa kocha aliyezipandisha timu ligi kwa miaka miwili mfululizo.
Msimu uliopita aliipandisha Singida United inayoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu na safari hii amefanya mambo ya KMC. Hiki ni zaidi ya kismati unaambiwa.
Mwanaspoti limemdaka kocha huyo na kupiga naye stori mbili tatu na kufunguka siri ya mafanikio yake.
MIPANGO ILIKAA VEMA
Minziro anasema Ligi Daraja la Kwanza ina changamoto kuwa kwa vile ni ligi yenye mechi chache, hivyo inakupasa upigane katika kila mechi ili uweze kusogea mbele katika hatua nyingine.
“Huku sio kama VPL, huku ukipoteza sana katika michezo yako shughuli unakuwa huna tena, inabidi upambane ushinde katika kila mechi ili upande, au ushinde mechi za nyumbani.”
Pia Minziro aligusia changamoto nyingine ilikuwa baada ya kupokonywa pointi, wachezaji wake walikata tamaa lakini aliweza kuwaaaminisha ubingwa ni lazima.
“Tulivyopokonywa pointi hakuna ambaye alikuwa sawa kiakili, nilijitahidi kuficha hisia zangu kwa wachezaji, nikawaambia tupambane mechi zinazokuja na bado tupo katika ushindi na huu ndio mpango uliotubeba,” anasema.
MECHI ZA KIRAFIKI
Minziro anadai kucheza mechi nyingi za kirafiki na klabu za Ligi Kuu, zilimsaidia vilivyo kuingia katika mbio za kupanda daraja.
“Nilicheza na Simba, Yanga na Azam, hizi zote zipo vizuri katika VPL, hivyo nilikuwa nachota ujuzi kwao na kukipima kikosi changu vizuri. Mechi hizi zilinifanya niweze kuona matatizo ya kikosi changu na kufanya marekebisho kwa haraka na kikosi kikawa bora,” anasema.
UONGOZI BORA
Timu nyingi za Ligi Daraja la Kwanza, huwa zipo katika changamoto kubwa katika upande wa uongozi, hasa katika nyanja mbalimbali katika kuihudumia timu.
Minziro anasema; “Viongozi wangu walikuwa bega kwa bega hasa Mstahiki Meya wa Kinondoni kwani, tulikuwa tunaweka kambi sehemu nzuri, tulikwenda mpaka Zanzibar kwa ajili ya kambi.”
Anaongeza kuwa, sababu kama hizo za uongozi bora ndizo zilizoisaidia hata Singida United kupanda Ligi Kuu ya msimu huu ikiwa chini yake.
TUKIO LA FURAHA
Minziro alicheka kidogo kisha akasema walipopokonywa pointi na kupewa Mlale kisha na wao kwenda kuchukua pointi hizo kihalali kwa ushindi ni tukio la furaha katika ligi hiyo.
“Furaha yangu ni kwamba tulipokonywa pointi nyuma huko, lakini sisi tukaenda kuchukua pointi zetu tatu kwa ushindi sehemu ile ambayo pointi zetu zilienda hivyo tumezirejesha,” anasema Minziro ambaye amefunguka kuwa anaichukulia kwa umakini mkubwa michuano ya Kombe la FA.
“Nataka kuhakikisha tunafuzu hatua ya 16 ya FA na mchezo wetu na Toto Africans bado hatujacheza, lakini nataka kufanya mambo makubwa kule ili tukae vizuri zaidi,” alisema.
MKATABA UPOJE
Wakati akiipandisha Singida United, kuliibuka vuguvugu la kimkataba na waajiri wake hao, hivyo Mwanaspoti lilitaka kufahamu kwa kina kuhusiana na hatma yake kwenye kikosi cha KMC.


“Kazi yangu niliyokubaliana nayo awali imeshakamilika, hivi sasa nasubiri tukae chini tena na uongozi wangu tujue tunafanyeje, kazi yangu ya awali nimekamilisha,” anasema.

Comments