Mgawanyiko baina ya Warepublican kuhusu waraka wa siri wa FBI.

Mgawanyiko baina ya Warepublican kuhusu waraka wa siri wa FBIMgawanyiko baina ya wajumbe wa chama cha Republican unaonekana kuwa mkubwa zaidi siku mbili baada ya Kamati ya Upelelezi ya Kongresi ya Marekani kutoa waraka wa siri wa Idara ya Upelelezi ya Federali (FBI) juu ya ushirikiano wa timu ya uchaguzi wa rais ya Trump na Russia.

Tofauti na mtazamo wa Rais Donald Trump wa Marekani anayetoka chama cha Republican, unaosisitiza udharura wa kusitishwa uchunguzi kuhusu faili la madai kuwa Russia iliingilia uchaguzi wa Rais wa Marekani, baadhi ya wajumbe wa chama cha Republican wanasisitiza udharura wa kuendelezwa uchunguzi huo. 
Brad Wenstrup na Trey Gowdy ambao ni wajumbe wa chama cha Republican katika Kongresi ya Marekani wamesema kuwa waraka wa siri uliowekwa wazi wa FBI haupaswi kusitisha uchunguzi wa mahakama kuhusu faili hilo. 
Baada ya kutoa ruhusa ya kuondolewa waraka huo uliozusha makelele mengi katika orodha ya mafaili ya siri, Donald Trump aliandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, waraka huo unakadhibisha kuwepo njama ya kushirikiana na Warussia katika uchaguzi wa rais na sasa kadhia hiyo inapaswa kukomeshwa.
Waraka wa siri uliofichuliwa na Kamati ya Upelelezi ya Kongresi ya Marekani unaashiria makosa yaliyofanywa na FBI na Mwanasheria Mkuu katika kunasa sauti za mjumbe wa kamati ya kampeni za uchaguzi ya Donald Trump hapo mwaka 2016 na juhudi za kamati ya kampeni za uchaguzi ya Hillary Clinton za kutaka kuthibitisha kuwa watu wa karibu na Trump walishirikiana na Warussia. Waungaji mkono wa Donald Trump katika Kongresi akiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Upelelezi, Devin Nunes wameamua kuweka wazi waraka huo wa FBI ili kuthibitisha kwamba, timu inayoshughulikia faili la Trump-Russia ilikiuka sheria na msingi wa kutopendelea upande wowote. 
Hata hivyo mbali na Wademocrat ndani ya Kongres, idadi kadhaa ya wabunge wa chama tawala cha Republican pia wanapinga suala la kusitishwa uchunguzi wa faili la Trump-Russia unaosimamiwa na mkaguzi maalumu wa faili hilo, Robert Mueller. 
Kwa mfano tu wabunge Chris Stewart na Will Hurd wa chama cha Republican wanasisitiza kuwa, uchunguzi huo unapaswa kuendelea na kwamba Wizara ya Sheria na Idara ya Upelelezi wa Federali (FBI) zinapaswa kuendeleza kazi zao za uhakiki. 
Misimamo kama hiyo inafunga mikono na miguu ya White House na waungaji mkono wa Trump ndani ya Kongresi wanaotaka kuzuia uchunguzi wa Robert Mueller katika faili la Trump-Russia. 
Kwa sasa kumejitokeza mgawanyiko mkubwa baina ya Warepublican juu ya suala la kumtetea Rais Donald Trump na suala la madai ya uingiliaji wa Russia katika siasa za Marekani. 
Mrengo wenye nguvu kubwa uliodhidi ya Russia nchini Marekani ambao pia umepenya na kuwa na ushawishi mkubwa baina ya Warepublican, unafanya jitihada za kutumia maudhui ya uchaguzi wa rais wa mwaka 2016 kama turufu ya kukabiliana na Russia na kuharibu kabisa uwezekano wa aina yoyote wa kuboreshwa uhusiano wa Washington na Moscow.
Kwa sababu hiyo waraka ambao waungaji mkono wa Trump walikuwa wakitarajia kwamba, utakuwa mwanzo na msingi wa kukomeshwa uchunguzi wa Mueller, sasa umekuwa kaa la moto kwa Warepublican wenyewe na kwa mwenendo huu yumkini ukamburuta kikamilifu Rais Donald Trump katika faili la kushirikiana na Russia katika uchaguzi uliopita wa rais nchini Marekani.    
Chanzo:parstoday.

Comments