Mapya yaibuka kuhusu Tshabalala.


MSIMU uliopita beki wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alikuwa ndiye habari ya mjini kwani licha ya kucheza dakika zote 2,700 za msimu, alichaguliwa pia kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Bara.
Msimu huu staa huyo wa zamani wa Azam na Kagera Sugar, amejikuta akisugua benchi tofauti na matarajio ya wengi huku baadhi ya mashabiki wakimshutumu kuwa ameshuka kiwango, lakini kumbe kuna siri nyingine nyuma ya anguko la beki huyo anayetajwa kuwa na nidhamu ya hali ya juu Msimbazi.
Kwa sasa nafasi yake inachezwa na Mghana, Asante Kwasi, aliyejiunga na Simba wakati wa usajili wa dirisha dogo akitokea Lipuli ya Iringa.
Imeelezwa kuwa mfumo wa 3-5-2 unaotumika Msimbazi kwa sasa, ndio unaombana Tshabalala kwani Kwasi ndiye anayefiti zaidi kwenye mfumo huo.
Kocha wa zamani wa Yanga, Kenny Mwaisabula, anafafanua kuwa Kwasi na Tshabalala ni wazuri, lakini tofauti yao ipo kwenye umiliki wa mipira ambapo Tshabalala anashindwa kuumiliki vizuri hivyo kujikuta akiachwa nyuma.
“Tshabalala hana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira ukimlinganisha na Kwasi, hii ndio sababu kubwa inayopelekea makocha wamuanzishe benchi maana wanapata faida nyingi kwa Kwasi. 
Kikubwa ambacho kinaweza kumsaidia Tshabalala kwa sasa ni kujiongeza na kujitambua kwamba nini anapaswa kufanya ili arudi kama awali,” alisema Mwaisabula.
Naye kocha, Joseph Kanakamfumu, alisema: “Simba ilikuwa haijapata mtu sahihi wa kucheza namba tatu, ndio maana Tshabalala aling’aa zaidi, ila msaada wake haukuwa mkubwa. Ni tofauti na ilivyo kwa Kwasi.
“Tatizo la Tshabalala hana uwezo mkubwa wa kupiga krosi, kutoa pasi za mwisho. Mambo hayo Kwasi anayaweza zaidi.”
chanzo:Mwanasport.

Comments