Leo ni siku ya Alkhamisi tarehe 15 Februari 2018.

Alkhamisi tarehe 15 Februari 2018Leo ni Alkhamisi tarehe 28 Jamadil Awwal 1439 Hijria sawa na Februari 15, 2018.

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, Jeshi Jekundu la Shirikisho la Urusi ya zamani lililazimika kuondoka nchini Afghanistan baada ya kuikalia kwa mabavu nchi hiyo kwa miaka kumi. 
Majeshi hayo yaliondoka baada ya kushindwa kukabiliana na mapambano ya mujahidina wa Kiislamu. 
Lengo la Umoja wa Sovieti la kuivamia na kuikalia kwa mabavu Afghanistan mwaka 1979, lilikuwa ni kuizatiti na kuitia nguvu serikali kibaraka ya Kabul iliyokuwa ikiungwa mkono na Moscow na kueneza satua yake upande wa maeneo ya kusini mwa Asia. 
Hatua hiyo iliyoyatumbukiza hatarini maslahi ya Marekani, ilikabiliwa na radiamali kali ya Washington ambapo Ikulu ya Marekani (White House) ilianzisha operesheni za kuyatoa majeshi ya Umoja wa Sovieti huko Afghanistan. 
Hatimaye baada ya miaka 10 wananchi wa Afghanistan wakisaidiwa na Mujahidina walifanikiwa kuhitimisha uvamizi huo na kuyatoa majeshi ya Urusi katika ardhi yao.
Miaka 120 iliyopita na katika sikukama ya leo, Mirza Muhammad Hassan Shirazi, mmoja wa wanazuoni wakubwa na mashuhuri wa Kiislamu aliaga dunia. 
Alizaliwa Shiraz huko kusini mwa Iran na baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kuendeleza masomo yake ya kidini na kupata elimu kwa wanazuoni mashuhuri wa mji huo kama Sheikh Murtadha Ansari. 
Bidii yake kwenye masomo ilimuwezesha kukwea haraka daraja za elimu na kuwa mhadhiri na mwanazuoni wa ngazi za juu mjini hapo na katika ulimwengu mzima wa Kiislamu. 
Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatuwa yake ya kuharamisha tumbaku katika kipindi cha utawala wa Nassiruddin Shah kutoka ukoo wa Qajaar. 
Fatuwa yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa ikihodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. 
Fatuwa hiyo ilitambuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingereza nchini Iran. 
Kwa hakika hatua hiyo iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni nchini.
Miaka 236 iliyopita vilianza vita vya majini kati ya Ufaransa na Uingereza katika pwani ya India. 
Vita hivyo vilivyodumu kwa muda wa miezi saba, vilikuwa ni mlolongo wa vita kati ya nchi mbili hizo vilivyokuwa na lengo la kuikoloni India na kupora utajiri wake. 
Ijapokuwa Ufaransa ilishinda vita hivyo, lakini nchi hiyo haikuweza kurejea India na kuikoloni nchi hiyo, na badala yake Uingereza ilibaki na kuendelea kuwa mkoloni mkuu huko Bara Hindi.
Siku kama ya leo miaka 454 iliyopita alizaliwa msomi mashuhuri, mnajimu na mtaalamu wa fizikia wa Italia, Galileo Galilei katika mji wa Pisa. 
Alisoma fasihi hadi alipokuwa na umri wa miaka 19 na baadaye akajishughulisha na fizikia na hisabati. 
Galileo alitumia lenzi iliyovumbuliwa na msomi na mnajimu mashuhuri wa Kiislamu Ibn Haitham kutengeneza darubini ya elimu ya nujumu kwa ajili ya kutazamia nyota na sayari. 
Galileo alitumia chombo hicho kuthibitisha kwamba sayari ikiwemo ya ardhi, zinazunguka jua. 
Utafiti huo wa Galileo Galilei ulithibitisha nadharia ya msomi Muislamu wa Iran ambaye karne kadhaa kabla yake alithibitisha kwamba ardhi inazunguka jua. 
Baada ya kusambaa nadharia hiyo ya Galileo kuhusu mzunguko wa ardhi na sayari nyingine kando ya jua, kanisa la Roma lilimtuhumu kuwa kafiri na kupelekea kuhukumiwa kifungo cha maisha cha nyumbani. 
Baadaye msomi huyo alilazimika kukanusha nadharia hiyo kwa ajili ya kuokoa maisha yake.
 Hii nikwahisani ya parstoday.

Comments