Leo ni Alkhamisi tarehe 8 Februari, 2018.

Leo ni Alkhamisi tarehe 8 Februari, 2018Leo ni Alkhamisi tarehe 21 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1439 Hijria sawa na Februari 8, 2018.

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita wananchi wa Iran walifanya maandamano makubwa katika miji mbalimbali ya Iran na kusisitiza juu ya kuendelezwa mapambano hadi kuuangusha utawala wa Shah. 
Mamilioni ya wananchi Waislamu wa Iran waliandamana katika siku kama hii wakijibu wito wa Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu aliyewataka waiunge mkono serikali ya muda ya Mapinduzi. 
Katika upande mwingine maafisa na vikosi vya Jeshi la Anga la Iran huku vikiwa katika sare zao za kijeshi, walielekea kwa Imam na kutangaza mshikamano wao na Mapinduzi ya Kiislamu na uongozi wa Imam Khomeini. 
Katika mazungumzo hayo, Imam Ruhullah Khomeini aliwaambia wanajeshi hao kwamba walikuwa watumishi wa utawala wa kitaghuti na sasa wamejiunga na Qur'ani. 
Hatua ya vikosi vya Jeshi la Anga la Iran ya kutangaza utiifu wao kwa Imam Khomeini iliukasirisha sana utawala wa Shah.
Tarehe 8 Februari miaka 55 iliyopita Kanali Abdu Salam Arif alifanikiwa kushika hatamu za uongozi nchini Iraq, baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu akishirikiana na maafisa wa kijeshi wa Chama cha Baath. 
Akisaidiwa na majeshi ya anga ya Iraq, Kanali Abdu Salam Arif alilishambulia jengo la Wizara ya Ulinzi ya Iraq yalipokuwa makao ya Abdul-Karim Qassim, Rais wa wakati huo wa nchi hiyo. 
Baada ya kumtia mbaroni na kumuua Rais huyo, Abdu Salam Arif alijitangaza kuwa Rais wa nchi hiyo. 
Abdul-Karim Qassim alikuwa ameingia madarakani mwaka 1958, baada ya kufanya mapinduzi ya umwagaji damu dhidi ya mfalme wa mwisho wa Iraq. 
Kanali Abdul Salam Arif alifariki dunia mwaka 1966 katika tukio la kutatanisha la ajali ya helikopta, na kaka yake yaani Abdul-Rahman Arif akawa Rais wa Iraq.
Na miaka 1119 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 21 Mfunguo 8 mwaka 320 Hijiria, alizaliwa Abu Jaafar Ahmad bin Ibrahim Qiravani, katika mji wa Shirvan ulioko kaskazini mashariki mwa Iran. 
Msomi huyo alijulikana kwa jina maarufu la Ibn Jazzar, na alikuwa tabibu, mwanafalsafa na mwanajiografia mashuhuri wa Kiislamu. 
Ibn Jazzar alikuwa tabibu mwenye moyo wa kujitolea na anayewatakia watu mema na aliandika kitabu kiitwacho "Twibul Fuqaraa” au Tiba ya Watu Maskini." 
Mwanafalsafa huyo ameandika vitabu 20. 
Miongoni mwa vitabu vyake ni Risalatun Fii Ibdalil Adwiya na Zadul Musafir.
 Hii ni kwahisani ya parstoday.

Comments