
Kukamatwa kwa mbunge huyo wa upinzani kunajiri wakati ambapo serikali imefunga vituo vitatu vya runinga mbali na vile vya redio.
Tom Kajwang alikamatwa na kundi la maafisa wa polisi waliokuwa wamevalia nguo za kiraia, mjini Nairobi.
Kukamatwa kwa kiongozi huyo kunajiri muda mfupi baada ya onyo kutoka
kwa waziri wa usalama kwamba watu waliohusika katika kumuapisha Raila
Odinga watakamatwa na kushtakiwa.
Vituo kadhaa vya runinga nchini Kenya vimefungiwa baada ya mamlaka ya
mawasiliano kuzima mitambo yao kwa kujaribu kupeperusha moja kwa moja
mkutano huo wa upinzani.
Sherehe ya kuapishwa kwa Raila ilichukuliwa kama mzaha lakini
serikali imeshikilia kuwa ni kitendo cha uhaini na kuhakikisha taarifa
hiyo haitawafikia Wakenya wengi waliokuwa wakiifuatilia tukio hilo.
Waziri wa usalama nchini Kenya Dr Fred Matiangi amesema kuwa runinga
hizo zitaendelea kufungwa hadi uchunguzi kuhusu kuhusika kwao na kundi
la pingamizi dhidi ya serikali NRM linalohusishwa na muungano wa Nasa
alilolipiga marufuku utakapokamilika.
Vifaa vya kurusha matangazo vya vituo vya runinga vya Nation Media
Group NTV, Citizen TV cha kampuni ya Royal Media services Limited na KTN
vilizuiwa kurusha matangazo katika kituo cha kurusha matangazo cha
Limuru huku kituo cha kitaifa cha KBC na K24 kinachohusishwa na Rais
Uhuru Kenyatta vikiendelea na matangazo yao.
Tangazo hilo la Matiangi linajiri huku kukiwa na malalamishi miongoni mwa raia kufuatia hatua hiyo ya serikali.
Katibu mkuu wa shirika la wafanyikazi nchini Kenya COTU Francis
Atwoli ameishutumu serikali kwa kuingilia uhuru wa vyombo vya habari.
Bwana Atwoli ambaye alizungumza mjini Nairobi amesema kuwa hatua hiyo
ni kinyume na sheria na inaenda kinyume na katiba ya Kenya ambayo
inatoa Uhuru wa vyombo vya habari na kupata habari.
”Serikali inafaa kuharakisha na kurejesha matangazo ya
runinga hizo. Sio makosa tu bali pia ni kinyume cha katiba kuendelea na
biashara yao ya kuwahabarisha Wakenya”, alisema Atwoli.
Kufungwa kwa vituo hivyo kunajiri baada ya mwenyekiti wa shirika la
wahariri Kenya Linus Kaikai kudai kwamba rais Uhuru Kenyatta alikuwa
ametishia kuvifunga vyombo vya habari vitakavyojaribu kupeperusha
matangazo ya kuapishwa kwa viongozi wa NASA.
Kulingana na Kaikai , vitisho hivyo vilitolewa katika ikulu ya rais
tarehe 26 Januari baada ya wamiliki wa vyombo vya habari kuitwa na
kutakiwa kutorusha matangazo hayo.
Chanzo BBC.
Comments