Iran yajibu tuhuma za Marekani: Siasa zenu ndio chanzo hasa cha kuvurugika uthabiti Mashariki ya Kati.

Iran yajibu tuhuma za Marekani: Siasa zenu ndio chanzo hasa cha kuvurugika uthabiti Mashariki ya KatiOfisi ya Uwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imetoa jibu kwa tuhuma za balozi wa Marekani katika umoja huo na kueleza kuwa: uungaji mkono wa kila hali kwa siasa za kichokozi na uvamizi za utawala wa Kizayuni ndio chanzo kikuu cha machafuko na ukosefu wa amani katika Mashariki ya Kati.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya uwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imebainisha kuwa: wakati ukweli halisi wa mambo unaonyesha kuwa Iran imekuwa ikifanya jithada za dhati za kuondoa mivutano nchini Syria, serikali ya Marekani ndiyo inayokwamisha kila jitihada zinazofanywa kuhusiana na suala hilo.
Mbali na taarifa hiyo kusisitiza kwamba mchango na nafasi ya Marekani katika kuliimarisha kundi la kitakfiri la Daesh na ugaidi katika eneo haiwezi kukanushika, imebainisha kuwa chokochoko na uingiliaji wa kinyume cha sheria unaofanywa na Marekani katika nchi mbalimbali hususan, Iraq, Libya, Syria, Lebanon na Afghanistan umevuruga uthabiti katika nchi hizo na kulisababishia eneo maafa na masaibu.
Ikumbukwe kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja tangu Nikki Haley awe balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, mwakilishi huyo wa Washington katika UN ameshuhudiwa mara kadha wa kadha akiuunga mkono utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, ambapo katika kikao cha jana Jumatano cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichoizungumzia Syria alizusha tuhuma dhidi ya Iran na Russia kuwa eti zinavuruga uthabiti wa eneo.
Haley ametoa matamshi hayo dhidi ya Iran kufuatia kutunguliwa na kuangushwa na jeshi la Syria ndege ya kivita ya Israel iliyovamia anga ya nchi hiyo.
Kuangushwa ndege hiyo ya kivita ya utawala vamizi wa Israel kumeukasirisha utawala huyo haramu na muungaji mkono wake wa jadi Marekani.
chanzo:parstoday.

Comments