
Chama cha waandishi wa habari nchini Uganda kimeeleza hofu kuhusu
jinsi wanahabari wanavyoendelea kukamatwa na kufunguliwa mashtaka ya
uhaini.
Taarifa hiyo iliyotolewa jana na chama hicho imejiri baada ya
waandishi wa habari watatu wa gazeti wa Daily Monitor kukamatwa katika
mazingira ya utatanishi na kushtakiwa kwa njama ya kujaribu kuipindua
serikali, mashtaka ambayo adhabu yake ni kifo endapo watakutwa na hatia.
Nchini Uganda kumekuwa na ripoti za waandishi wa habari kutekwa na
watu wasiojulikana na kisha baadaye kupatikana gerezani wakiwa
wamefungwa bila hatia kumezua hofu kubwa kwa waandishi wa habari.
Jana Jumatatu Februari 19, 2018 mwandishi wa habari wa kituo cha
habari cha kibinafsi cha Top Radio, Richard Kasule alikamatwa nje ya
ofisi za kituo hicho muda mfupi baada ya kuandaa matangazo ya asubuhi.
Wafanyakazi wenzake katika kituo hicho cha habari walidai kwamba
Kasule alikamatwa na polisi baada ya kufichua ushirikiano kati ya
walinda usalama na makundi ya uhalifu jijini Kampala.
Mtangazaji huyo aliandaa kipindi cha saa nzima akiwahoji viongozi wa
makundi hayo ya uhalifu waliodai kushirikiana na polisi katika uhalifu.
Hatua ya kukamatwa kwa kasule inajiri siku mbili baada ya mwandishi
wa gazeti la serikali la the New Vision, Charles Etukuri, kukamatwa nje
ya ofisi za gazeti hilo la serikali.
Etukuri alichapisha taarifa ya upekuzi kuhusiana kifo cha mwekezaji
kutoka bara la Ulaya katika hoteli moja maarufu jijini Kampala, na
kukamatwa kwa viongozi wakuu 6 wa polisi kisiri.
Mwandishi mwingine wa habari, Isaac Bakka, alipatikana gerezani baada
ya kutoweka katika mazingira ya kutatanisha wiki mbili zilizopita.
Hata hivyo, Mahakama jijini Kampala kupitia Mkurugenzi wa Habari,
Solomon Muyita, amesema mwandishi huyo alikuwa ameshafunguliwa mashtaka
ya uagizaji wa silaha hatari kwa nia ya kuipindua serikali ya Yoweri
Museveni.
Wahariri wa gazeti la upekuzi la Red Pepper, Juice FM na gazeti
linalochapishwa kwa lugha ya kiganda la ‘Kamunye,’ nao wanakabiliwa na
mashtaka ya kujaribu kuipindua serikali ya rais Yoweri Museveni.
Vituo hivyo vimefunguliwa hivi majuzi baada ya kufungiwa kwa mda wa
mwezi mmoja kwa makosa ya kuandika habari za kichochezi na zenye lengo
la kuvuruga amani nchini humo.
Chanzo:VOA na zanzibar24.
Comments