Akizungumza jana usiku huko Amman mji mkuu wa Jordan kabla ya safari yake nchini Lebanon, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema: Lazima tukubali kuwa Hizbullah ni sehemu ya mchakato wa kisiasa wa Lebanon.
Tillerson ametoa kauli hiyo katika hali ambayo Marekani imeiweka Hizbullah kwenye orodha ya makundi ya kigaidi kwa sababu tu ya msimamo wa harakati hiyo ya muqawama wa kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel na makundi ya kigaidi katika Mashariki ya Kati. Kwa mtazamo wa Washington, hatua hizo za Hizbullah ni haribifu kwa maslahi ya Lebanon na eneo.
Ikumbukwe kuwa harakati ya Hizbullah iliasisiwa mnamo miaka ya 1980 kufuatia hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel kulivamia na kulikalia kwa mabavu eneo la kusini mwa Lebanon.
Harakati hiyo iliendesha mapambano makali yaliyoulazimisha utawala huo haramu uondoke kimadhila katika eneo hilo mwezi Mei mwaka 2000.
Harakati hiyo ambayo sasa imekuwa mhimili wenye nguvu kubwa kijeshi na kisiasa ndani ya Lebanon ulitoa kipigo kingine kikali kwa Israel katika vita vya mwaka 2006 ilivyoanzisha dhidi ya Lebanon.
Awali Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza kuwa suala la Hizbullah itakuwa ajenda kuu ya mazungumzo atakayofanya Tillerson na viongozi wa Lebanon wakati wa safari yake nchini humo anayotazamiwa kufanya hii leo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Lebanon Michel Aoun, Waziri Mkuu Saad Hariri na Spika wa Bunge Nabih Berri.
Katika safari yake ya kuzitembelea nchi kadhaa za eneo ambazo ni Misri, Jordan, Lebanon, Kuwait na Uturuki, siku ya Jumapili Rex Tillerson aliwasili Cairo mji mkuu wa Misri.
chanzo:parstoday.
Comments