YANGA imecheza mechi zake kadhaa bila mastraika wake nyota akina Amissi Tambwe, Donald Ngoma, Ibrahim Ajibu na Yohana Mkomola na mashabiki wake bado hawajui ni lini janga la majeruhi litaisha katika timu yao ili waendele kula raha.
Hata hivyo kiungo Pius Buswita aliyeifungia timu hiyo mabao matatu katika Ligi Kuu Bara likiwamo lile la juzi Jumamosi mjini Iringa, amewajaza upepo mashabiki hao kuwaambia kuwa watulie kwani ataendelea kutupia kila akipata nafasi.
Buswita alisema licha ya kwamba kiasili ni kiungo, lakini hata kwenye namba ya Tambwe yeye anamudu kuicheza na kama akipewa nafasi atatupia kwani amekuwa akijifua kivyake ili kumudu nafasi ya ushambuliaji na Yanga haipaswi kuwa na hofu.
Mchezaji huyo aliyesajiliwa msimu huu kutoka Mbao FC, alisema anajitofautisha na viungo wenzake kwa kuwa mwepesi wa kufunga na hii ni kwa sababu huwa anafanyia mazoezi jambo hilo, hivyo ataendelea kufunga tu.
“Naweza kucheza kama mshambuliaji hivyo hata kucheza anapocheza Tambwe mi namudu vizuri tu, hata ninapokuwa mazoezi huwa najifunza kufunga ndio maana ninapofika sehemu ya kufunga huwa siwaachi makipa,” alisema Buswita.
Aliongeza huwa anafunga kirahisi kwa sababu ya kutumia miguu yote na kichwa vitu ambavyo hata Tambwe amekuwa akifanya hivyo na kutisha kwa mabao katika Ligi Kuu tangu atue mwaka 2013 japo hali ya kuwa majeruhi safari hii inamzingua.
“Najituma na kuongeza umakini hasa ninapofika eneo la ushambuliaji, nafunga kwa njia zote, hivyo naamini kabisa nikiendelea kufanya hivi naweza kabisa kuingia katika orodha ya wafungaji bora msimu huu na kubeba tuzo,” alisema.
Tambwe ndiye mchezaji aliyenyakua Tuzo ya Mfungaji Bora mara nyingi miongoni mwa wachezaji wa Yanga akifanya hivyo tangu akiwa na Vital’O ya kwao Burundi, Simba na hata alipotua Yanga akitwaa msimu wa 2015-2016
Mzambia akiri
Katika hatua nyingine Kocha Mkuu wa Yanga, George Lwandamina, amekiri kuwa licha ya ushindi wa mabao 2-0 walioupata Iringa juzi mbele ya Lipuli, lakini hakutulia kitini kutokana na makosa yaliyokuwa yakifanywa na vijana wake hasa mabeki.
Lwandamina aliyewachezesha Gadiel Michael na Hassan Kessy pembeni na kati kuwaweka Kelvin Yondani ‘Vidic’ na Juma Said ‘Makapu’, alisema timu haikumpa amani katika muda wote wa pambano hilo lililopigwa Uwanja wa Samora.
“Mechi ilikuwa nzuri na tunashukuru tumeshinda, lakini pamoja na hilo, hatukuwa vizuri sana katika kuzuia, tulikuwa tunafanya makosa ya hapa na pale,” alisema.
Yanga tayari imerejea jijini Dar es Salaam tangu jana kwa ajili ya kuwahi pambano lao lijalo kesho Jumanne dhidi ya Njombe Mji, ikipambana kuifukuza Simba .
Matokeo hayo yameifikisha pointi 31 na kukamata nafasi ya tatu nyuma ya Azam yenye alama 33 na Simba inayoongoza kwa pointi 38 baada ya jana kuibwaga Ruvu Shooting 3-0.
Comments