Nabil Shaath, mshauri wa Rais Mahomud Abbas wa Mamlaka ya ndani ya Palestina katika masuala ya kimataifa amesema, mamlaka hiyo imeikabidhi Mahakama ya ICC mafaili ya kesi za jinai zilizofanywa na utawala ghasibu wa Kizayuni zikiwemo za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kwamba mafaili hayo hivi sasa yanapitiwa na kuchunguzwa na mahakama hiyo.
Shaath ameongeza kuwa: sambamba na kuendelea uafriti wa Wazayuni, wa kuhalifu sheria za kimataifa na kuendeleza sera za ujenzi wa vitongoji pamoja na kupuuza maazimio ya Umoja wa Mataifa, timu ya uongozi wa Palestina iko tayari kuivunja Mamlaka ya Ndani ya Palestina, ili Israel, ukiwa ni utawala ghasibu na vamizi ubebe dhima na mas-ulia kamili ya uendeshaji wa ardhi ya Palestina.
Kiongozi huyo mwandamizi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amebainisha kwa kusema: kwa hatua hii, gharama na dhima ambayo tunaibeba sisi hivi sasa itaielekea Israel.
Nabil Shaath amesisitiza kuwa ujenzi wote wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ni haramu na uko kinyume na sheria na vitongoji hivyo inapasa viondolewe.
Siku ya Jumatatu iliyopita, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na viongozi wa Marekani kuwataarifu uamuzi wa utawala huo haramu wa kuviweka chini ya mamlaka yake kamili vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vilivyoko kwenye eneo la Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan.
Comments