Yanga bila mastaa yaitolea macho Mwadui.

Mshambuliaji wa Yanga, Amiss Tambwe (kushoto)

Dar es Salaam. Wakati Yanga ikiteremka uwanjani leo kuvaana na Mwadui, mchezo huo utashereheshwa na mabingwa hao kuingia mkataba wa udhamini wa Sh2 bilioni na kampuni ya Marcon.
Yanga inayoshika nafasi ya tano katika msimamo wa ligi itavaa Mwadui katika mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara watakosa huduma ya nyota wake Donaldo Ngoma, Amissi Tambwe, Thabani Kamusoko, Geofrey Mwashiuya wote ni majeruhi na Obrey Chirwa ambaye amefungiwa mechi tatu.
Hata hivyo, Yanga inatakiwa kuwa makini na Mwadui inayoshika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na  pointi 12. Yanga ina pointi 21 ikiwa nafasi ya tano.
Nahodha wa Mwadui, Paul Nonga, amebeba jahazi la timu yake katika kuhakikisha wanashinda mchezo huo.
Nonga anaifahamu vyema Yanga kwa kuwa aliwahi kuitumikia misimu miwili kabla ya kutimkia Mwadui.
Mshambuliaji huyo atacheza mchezo huo akiwa na rekodi ya kufunga mabao mawili katika mchezo uliopita dhidi ya Ruvu Shooting walioshinda 2-1.
Mabeki wa Yanga, Kelvin Yondani na Andrew Vincent watakuwa na kazi ngumu ya kumdhibiti Nonga ambaye ndiye mfungaji bora wa Mwadui msimu huu.
Kocha msaidizi wa Mwadui, Jumanne Ntambi alisema hakuna mchezaji wa Yanga wanayemuogopa ingawa watacheza kwa tahadhari ili kupata ushindi.
“Najua Yanga imetoka kujeruhiwa ilikutana na kipigo kutoka kwa Mbao kwenye ligi halafu ikatolewa Kombe la Mapinduzi, lazima watacheza kwa nguvu kupata ushindi.
“Nina wachezaji wengi wazuri na wazoefu ambao naamini kama watacheza kwa kiwango bora ushindi utapatikana,”alisema Ntambi.
Yanga ina rekodi bora dhidi ya Mwadui Dar es Salaam baada ya kushinda mechi zote mbili. Timu hiyo ilishinda mabao 2-1 mwaka 2016 na 2017 ilishinda 2-0.
Kocha msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa alisema wamejindaa vizuri kushinda mchezo huo ili kujiweka pazuri kwenye msimamo wa ligi.
Wakati huo huo, Yanga imeingia mkataba wa miaka mitatu, wenye thamani  ya zaidi ya Sh2 bilioni na kampuni ya kutengeneza vifaa vya michezo ya Macron.
Katibu mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa alisema mkataba huo utakuwa na ongezeko kila mwaka kutokana na mauzo ya jezi na vifaa mbalimbali vya michezo.
“Tumeingia mkataba wa miaka mitatu na kampuni ya Macron wenye thamani ya Sh2 bilioni kutengeneza vifaa vya michezo ikiwemo jezi  za mechi na mazoezi.
Mwakilishi wa kampuni ya Macron, Suleiman Karim alisema ni faraja kuingia mkataba na Yanga, hivyo jukumu lao ni kuhakikisha wanatengeneza vifaa muhimu katika ubora wake.

Comments