Waislamu Nigeria wasisitiza serikali imuachilie huru Sheikh Zakzaky.

Waislamu Nigeria wasisitiza serikali imuachilie huru Sheikh ZakzakyHarakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) imesema hata baada ya serikali kueneza video iliyochujwa ya kiongozi wa harakati hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky, bado hawatatulia hadi pale mwanazuoni huyo atakapoachilia huru.

Katika taarifa siku ya Jumapili, Harakati ya Kiislamu Nigeria ilisisitiza kuwa itaendelea na maandamano ya amani ili kuishinikiza serikali imuachilie huru Sheikh Zakzaky.
Taarifa hiyo imesema Waislamu hawawezi kuridhishwa na sekunde chache za klipu ya video ya Sheikh Zakzaky ambaye anaendelea kushikiliwa kinyume cha sheria.
Sheikh Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambaye kwa miaka miwili sasa anashikiliwa kinyume cha sheria, siku ya Jumamosi, kwa mara ya kwanza alionekana hadharani akihojiwa na waandishi habari. Wakuu wa Nigeria walimruhusu Sheikh Zakzaky aonekane hadahrani baada ya kuenea uvumi kuwa amepoteza maisha akiwa kizuizini.
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inasisitiza kuwa serikali lazima itekeleze amri ya mahakama ya kumuachilia huru badala ya kujihusisha na sarakasi za kueneza klipu za video.
Itakumbukwa kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky akiwa na mke wake walitekwa nyara na Jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 wakati askari walipovamia kituo chake cha kidini huko katika mji wa Zaria jimboni Kaduna. Tokea wakati huo Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakizuiliwa katika mojawapo ya vituo vya kijeshi vya nchi hiyo bila kufunguliwa mashktaka.
Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo ambalo limenyamaziwa kimya na Umoja wa Mataifa.
chanzo:parstoday.

Comments