Taarifa ya Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Mataifa nchini
Libya UNSMIL imesema maafisa wa UN wameshtushwa na habari za kupatikana
miili mitano ya watu waliouawa katika kijiji cha Laithi mjini Benghazi,
huku mitatu ikipatikana katika eneo la Derna, yapataka kilomita 250
mashariki mwa mji huo wa pili kwa ukubwa nchini Libya.
UNSMIL imesema maiti za watu hao zina majeraha mengi yanayoonyesha
kuwa waliteswa kabla ya kufyatuliwa risasi. Imeongeza kuwa, kufikia sasa
haijabainika waliohusika na mauaji hayo.
Haya yanajiri siku chache baada ya watu wasiopungua 35 kuuawa na
wengine 70 kujeruhiwa katika miripuko miwili ya mabomu iliyotokea mjini
Benghazi.
Libya ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa na hali ya mchafukoge
tangu kupinduliwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi mwaka
2011, kufuatia uingiliaji kijeshi wa Marekani na waitifaki wake katika
Muungano wa Kijeshi wa Nchi za Magharibi (Nato).
Comments