Askofu
Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe
amejibu hoja zinazotolewa dhidi yake, baadhi zikitolewqa na Serikali
akisema anapozungumza ni lazima kutafakari kabla ya kumkabili.
Askofu Kakobe alizungumza jana wakati wa ibada katika kanisa la FGBF lililopo Mwenge jijini Dar es Salaam.
“Ukisikia Kakobe amezungumza, tafakari kwanza kabla ya kumkabili,” alisema.
Kauli hiyo aliitoa ikiwa ni siku moja baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutangaza kuanzakufuatilia ulipaji wake wa kodi.
Uamuzi
wa TRAulitangazwa juzi na Kamishna Mkuu, Charles Kichere mbele ya
waandishi wa habari baada ya hivi karibuni Askofu Kakobe kusikika
akisema ana fedha nyingi kuliko Serikali.
TRA
ilisema uamuzi huo unatokana na kiongozi huyo wa kiroho kutokuwemo
katika kumbukumbu za ulipaji kodi za mamlaka hiyo. Mamlaka hiyo ilisema
kama utajiri wake unatokana na sadaka pekee litakuwa jambo la kushtua.
Jana,
Askofu Kakobe alitumia ibada hiyo kuwajibu TRA na pia alizungumzia
mambo mengine mawili; uraia wake na onyo la Serikali la kuwataka
viongozi wa dini kutokuzungumzia masuala ya siasa.
“Tangu
nilipoitika wito huu miaka 30 iliyopita, sijawahi kufanya biashara
yoyote zaidi ya hii na kanisa hili halina mradi wowote wa kiuchumi.
Kakobe hana mradi wowote na kama yupo anayejua ajitokeze aseme nitampa
zawadi,” alisema Askofu Kakobe.
“Akaunti
yetu iko Benki ya NBC na iko chini ya Bodi ya Wadhamini, bodi ambayo
imesajiliwa Rita (Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini). Kwa hiyo, hao
wanaotaka kujua zaidi waende Rita wakaulize wajumbe wa bodi hii ni
akina nani na waende NBC kuona vyanzo vyetu vya mapato kama ni tofauti
na sadaka.”
Huku
akishangiliwa na waumini, alisema tatizo kubwa lililojitokeza nchini ni
watu kutafasiri wanavyojua na kujikuta wakipotoka. Alisema hilo ni
tatizo watu kutopenda kusoma Biblia kwa undani na kwa upana zaidi.
“Wamemsikia
Kakobe anazungumza hapa, anazungumza mambo ya rohoni kuhusu haya ya
utajiri. Unaweza kusikia maneno ukatafsiri kivyako kwa sababu haya
tunayozungumza hapa ni mambo ya rohoni, wewe unayatafsiri kisiasa,”
alisema Kakobe.
“Wanasema
wewe una hela kweli kuliko Tanzania sema... ninaweza kuvunja hekalu na
kulisimamisha kwa siku tatu. Mtu anajiuliza hekalu gani hili? Hekalu
hili ni mwili wake. Maana yake niueni, nisulubisheni, lakini nitakufa na
siku ya tatu nitafufuka, hii ndio hekalu, unatafsiri kwa akili.”
Kwa
sauti ya juu na yenye msisitizo, Askofu Kakobe alisema: “Kimsingi, mimi
si mtu tu tajiri kuliko Serikali, bali ni tajiri kuliko Serikali zote
duniani. Kwa hiyo ukisikia Kakobe amezungumza, tafakari kwanza kabla ya
kumkabili.”
“Hela
yote ya Serikali ya Tanzania au dunia nzima haiwezi kununua tiketi hata
moja ya Mbinguni. Mimi ni tajiri kuliko Serikali ya Magufuli (Rais John
Magufuli) au Serikali ya Trump (Rais wa Marekani Donald Trump),”
alisema.
Alisema
nyumba anayoishi iliyopo Kijitonyama karibu na Kituo cha Polisi
Mabatini jijini Dar es Salaam aliijenga miaka ya sabini na tangu wakati
huo hajawahi kujenga kokote na gari lake ni la kawaida.
Askofu Kakobe alisema maisha yake si ya kifahari kama wasemavyo watu.
Uraia wake
Kuhusu
uraia, Askofu Kakobe alisema wazazi wake walikuwa wakiishi Kakonko
mkoani Kigoma na baada ya kufariki walizikwa huko, huku uraia wake
ukifuatiliwa na ilibainika ni raia halali.
“Baba
yangu alikuwa mwalimu kwa kipindi kirefu, amefanya kazi Tanga,
Sumbawanga, Usukumani kwa Wanyamwezi, Tabora na Shinyanga. Miongoni mwa
watu tuliocheza pamoja katika utoto wetu ni Christopher Chiza, huyu
alikuwa waziri,” alisema Kakobe.
“Ukitaja
kwa jumla familia yetu, inajulikana miaka mingi. Walikwenda kuchunguza
uraia wangu na kujiridhisha pasina shaka na kusema huyu ni Mtanzania.
Kuna kipindi watu walikwenda mara tatu kijijini kwangu Kakonko
kuchunguza uraia.”
Waumini
wakiwa kimya wakimsikiliza, Askofu Kakobe alisema, ‘’ Nimezaliwa
Tanzania, wazazi wangu wamezaliwa Tanzania, mimi ni Mtanzania kwa hiyo
sitoki hapa, tutabanana hapa hana.”
“Baada
ya kuona, yote hayo, mara waende huku, waende huko waulize wazazi wangu
ambao wamefariki hivi karibuni na makaburi yapo kijijini na niliwaambia
makaburi wayaweke barabarani ili anayechunguza uraia wangu aanzie
pale,” alisema.
Alisema,
‘’Kila jambo chini ya mbingu kuna kusudi, kuna kusudi la Mungu mimi
kuzaliwa Tanzania, kwa hiyo wanaosema nimetoroka hawanisumbui kichwa.”
Kuhusu
taarifa za kutoroka nchini alisema: “Ninapokwenda na kurudi washirika
wa hapa wanajua. Kwa mfano safari ya mwisho ilikuwa Agosti (mwaka jana)
na tangu hapo sijasafiri. Niko hapa na haya mengine nayasikia
nimetoroka, hayanisumbui, ukiitwa majina si yako unasumbukia nini?”
chanzo:Mpekuziblog.
Comments