Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema mchakato wa kupata kocha mpya wa timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ unatarajiwa kuanza mwezi ujao.
Pia TFF imesema imefungua milango kwa kocha mwenye sifa kutoka Zanzibar kutuma maombi ya baada ya kutangaza utaratibu kuhusu mchakato wa kumpata mrithi wa Salum Mayanga.
Mkataba wa Mayanga unatarajiwa kumalizika mwezi ujao na TFF imeanza kusaka kocha mpya atakayeipa mafanikio Taifa Stars katika mashindano ya kimataifa.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Willfred Kidao alisema kamati ya ufundi itachambua kwa makini sifa na vigezo stahiki vya kocha anayetakiwa.
Kidao alisema mchakato huo utajumuisha kocha kutoka Zanzibar na amewatoa hofu wadau wa soka kuhusu utaratibu wa nafasi ya kocha msaidizi wa Taifa Stars kuwa atatokea visiwani humo kama ilivyokuwa awali.
"Kocha msaidizi alikuwa anatoka Zanzibar kama mkuu anatoka Tanzania Bara, utaratibu tunaendelea nao. Morocco (Hemed) aliondoka Stars baada ya Zanzibar kupewa uanachama wa CAF, wamenyang'anywa na nafasi ya Muungano inaendelea kama kawaida,"alisema Kidao.
Hata hivyo, habari za ndani zimedokeza kuwa TFF imeanza mchakato wa kusaka kocha wa kigeni kuifundisha Taifa Stars na atasaidiwa na Mtanzania.
Comments