Nashangazwa namna tusivyomheshimu john bocco mwenye mafanikio rundo zaidi ya wageni unaowajua.


MSIMU huu, mshambuliaji John Raphael Bocco amejiunga na Simba akitokea Azam FC. Uamuzi wake ulielezwa kubeba mambo kadhaa kama mabadiliko, changamoto mpya na kadhalika.

Lakini kikubwa tulielezwa Bocco hakutaka dharau kwa kuwa Azam FC ilikuwa imeingia katika utaratibu mpya wa kupunguza gharama. Hivyo wakati wa usajili, mambo hayakuwa kama zamani na yeye akaona anaweza kuondoka.

Kutua kwake Simba kulikuwa gumzo na sasa kumekuwa gumzo zaidi baada ya masuala kadhaa kujitokeza likiwemo lile la Azam FC kuendelea kufanya vizuri katika Ligi Kuu Bara na juzi, imefanikiwa kubeba ubingwa wa Kombe la Mapinduzi.



Kinachoshangaza sana kwa wapenda mpira wengi sehemu mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania, kuhama huonekana ni kama uadui, kukosea au kukomoana.

Sasa inaonekana kama Azam FC ilifanya vizuri kumtoa Bocco, inaonekana Bocco ni kama alikosea Simba na huenda akafeli. Hata baada ya Azam kuchukua Kombe la Mapinduzi, mijadala imekuwa Bocco na wenzake kama Aishi Manula, Erasto Nyoni na kadhalika kwamba wameondoka na ubingwa umepatikana.

Leo tujikite kwa Bocco ambaye huenda Watanzania wameshindwa kuitambua kazi yake alikotoka na hadi sasa. Jambo ambalo linaonyesha wengi huzungumza bila ya kujikumbusha angalau kidogo.

Angalia katika kikosi cha Simba ambacho wengi wanalalamikiwa kutocheza kwa kujituma, hapa napo unaweza kuiona tofauti ya Bocco kwamba ni mchezaji anayetaka kitu fulani na hakiwezi kuwa tofauti na mafanikio.

Nchi pekee ambayo watu wanaweza kuambukizwa lawama ni Tanzania. Maana kila mmoja analaumu hata asiyekuwa na hoja ya msingi, ili mradi kasikia mwingine analalamika.

Bocco amekuwa akiifanya kazi yake kwa juhudi na hauwezi kumuweka katika kundi la watu wanaojituma bila ya majibu yenye mafanikio.

Tangu ametua Simba, Bocco amecheza mechi 10 za Ligi Kuu Bara, tayari amepachika mabao manne.  Alikosa mechi mbili tu za ligi hiyo Simba ikiivaa Njombe Mji na Ruvu Shooting. Amecheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya African Lyon na KMC na ana mabao manne. Ana bao moja katika mechi ya Kombe la Shirikisho na mechi tatu za Kombe la Mapinduzi akiwa na bao moja pia.

Katika mechi zote, Bocco kafunga katika ligi kuu, kirafiki, Kombe la Shirikisho na Kombe la Mapinduzi. Huyu ndiye mtu ambaye baadhi wanaamini Simba imekosea kumsajili kwa kuwa anakuwa majeruhi sana au tayari amebandikwa ule “uzee” uliowamaliza wachezaji wengi sana wa Tanzania.


Huyu Bocco, huenda ni mshambuliaji mzalendo ambaye timu nyingi sana za Tanzania zikiwemo Simba na Yanga hazikuwahi kuwa naye.

Akiwa na Azam FC ambayo si Simba wala Yanga na bado haijawa timu kongwe kama ambavyo wengi wanataka iwe sasa, aliiwezesha kubeba makombe lukuki, naye akashinda mataji mengi binafsi.



Ulitaka Bocco abaki Azam FC ili achukue nini? Ubingwa wa Afrika? Kama unaona amekosea kuondoka Simba, basi yanaweza kuwa mawazo yako lakini vizuri pia ukaanika hoja zako ukiwa na takwimu.

Bocco amewahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akiwa na Azam FC, akabeba ubingwa Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na timu hiyo aliyopanda nayo daraja.

Acha hivyo, ameiwezesha kubeba Ngao ya Jamii, leo Azam FC wanafurahia ubingwa wa Mapinduzi na wengine wanamzodoa Bocco lakini wanasahau ndiye nahodha wa kwanza wa Azam FC kubeba ubingwa huo, tena alikabidhiwa na huyohuyo Rais wa Zanzibar, Ali Mohammed Shein.
 


Kama tuzo za mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara wa mwezi pia Bocco amebeba zaidi ya mara mbili. Huyu mtu bado unaona amekosea kuhama Azam FC?

Nakukumbusha, wakati Azam FC inabeba ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Bocco ndiye alikuwa nahodha wa kikosi. Sasa unataka abaki Azam FC na hasa kama anaona si sahihi akiwa anasubiri nini?

Siku Kocha Joseph Omog alipomtoa Shiza Kichuya, nafasi yake ikachukuliwa na John Bocco na mashabiki wa Simba wakaanza kulalama wakiona hana msaada, dakika chache akafunga bao la kwenye “kideo” na kuwafunga midomo, huenda ingekuwa siku nzuri ya kuanza kubadilika na kuamini kilicho sahihi.



Waungwana msimdharau Bocco kwa kuwa ni Mtanzania na kwa kipindi cha miongo miwili, inaonyesha ndiye mchezaji mwenye mafanikio zaidi hapa nchini akiwa hachezi Yanga au Simba.

Angalia rekodi uone kama kuna mchezaji aliwahi kuipandisha timu, akabaki nayo ligi kuu hadi kuipa ubingwa, akaipa ubingwa wa Kombe la Afrika Mashariki na Kati na Ngao ya Jamii na kadhalika. Hutapata zaidi ya Bocco ambaye, anapaswa apewe heshima yake.

Tukubali Bocco naye ni mwanadamu, hivyo kwa mnayoyasema, basi yafanyieni uchunguzi na kwa mchezaji mwenye mafanikio au anayejituma uwanjani, hauhitaji kuwa na darubini.

Jifunzeni kuthamini juhudi za wenzenu, jifunzeni kuwapa moyo wenzenu. Lakini mkumbuke pia kuwathamini wachezaji Watanzania bila kujali wanacheza timu ipi ni jambo jema na kama kukosoa iwe ya kujenga badala ya kukatisha tamaa tu.



Vipi hamumjui John? Nawakumbusha naye ni mwanadamu na hawezi kupatia kila siku na kama kupatia ndiyo kipimo bora pekee, basi angalieni na aliyoyafanya, wangapi unawaona bora hawajafanya kama yeye hadi hii leo wawe wa ndani na hata nje?


SOURCE: CHAMPIONI

Comments