Mvua zinazoendelea kunyesha mkoani Morogoro zimesababisha vifo vya watu wawili katika wilaya ya Kilosa huku ikiacha zaidi ya kaya 1734 zikikosa makazi baada ya nyumba kubomoka.
Pia, mvua hizo zimeathiri visima vifupi 22 na kusababisha zaidi ya wananchi 3800 wa kata saba kukosa huduma ya maji safi na salama, huku ng'ombe takribani 63 wakihofiwa kufa.
Akizungumza leo Januari 17, 2018 na wananchi kijiji cha Tindiga wilayani Kilosa, mkuu wa mkoa wa Morogoro Dk Steven Kebwe amesema mbali na vifo hivyo, miundombinu mbalimbali imeharibiwa.
Amewataja waliopoteza maisha kuwa ni Annastazia Mayunga (58) mkazi wa Folkland manispaa ya Morogoro ambaye alifukiwa na kifusi, Peter Katumani mkazi wa kijiji cha Munisagara Kilosa aliyesombwa na maji.
“Mvua iliyoleta maafa ilinyesha Januari 8 hadi 12 na mbali na kusababisha vifo imeharibu zaidi ya ekari 8652 za mpunga na mahindi na kuharibu reli ya kati kutoka Gulwe wilaya ya Mpwapwa mkoa wa Dodoma hadi Kilosa Morogoro.”amesema Dk Kebwe.
Amebainisha kuwa mafuriko hayo mkoani Morogoro yamesababishwa na kubomoka kwa tuta la mto Mkondoa kufuatia kunyesha kwa mvua kubwa katika mikoa ya Dodoma na Manyara.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Kilosa, Kessy Mkambala amesema mafuriko hayo yameathiri kata za Magomeni, Manzese, Tindiga, Mabwerebwere, Berega, Mkwatani, Kidete, Mbigili na Msowelo.
Mkambala amesema mafuriko hayo yamesababisha nyumba 331 kubomoka huku nyingine 1395 zikiingiliwa na maji.
Amesema kutokana na athari ya mvua hiyo, tani 39 za mbegu za mahindi, na tani 48.072 za mpunga zikihitajika ili kuwapatia wakulima kwa ajili ya kupanda lengo likiwa ni kukabiliana na ukosefu wa chakula msimu ujao.
Mbunge wa Kilosa, Mbaraka Bawazir ametoa msaada wa kilo 200 unga kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko.
“Wananchi wa kata ya Tindiga wameathirika zaidi na mafuriko baada ya nyumba 291 kubomoka na 981 kuzingirwa na maji kufuatia kaya 1275 zenye watu 4330,” amesema.
chanzo:Mwananhi.
Comments