
Amesema katika hali ya kawaida viongozi hao hawawezi kukurupuka,
kwa hiyo ni lazima kuna tatizo wameliona na kwamba kauli zao hizo
zinalenga kujenga Taifa, si kubomoa.
Mjadala huo umeibuka baada ya viongozi wa dini kutumia ibada za
sikukuu ya Mwaka Mpya kuikosoa Serikali, baadhi wakisema haiheshimu
utawala wa sheria, wananchi kutopewa uhuru wa kutoa maoni yao, viongozi
kukubali kukosolewa huku wengine walizungumzia kuhusu haki na amani.
Miongoni mwao ni Askofu Zachary Kakobe aliyeitaka Serikali
ibadilishe Katiba na kurudi kwenye mfumo wa chama kimoja kama inaona
ndio sahihi kuliko kuvinyima vyama vya upinzani nafasi ya kutekeleza
wajibu wao.
Baadaye Mamlaka ya Mapato (TRA) ilitangaza kuwa itachunguza utajiri
wake baada ya kusikika akisema kuwa ana fedha kuliko Serikali, huku
katibu mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani akiwataka viongozi wa dini
kuacha kuzungumzia siasa madhabahuni.
“Hata wakati wa utawala wa (Rais wa Awamu ya Nne,
Jakaya) Kikwete na (wa Awamu ya Pili, Ali Hassan) Mwinyi, viongozi wa
dini walikuwa wakitoa maoni yao na kusikilizwa,” alisema Maalim Seif.
Waziri kiongozi huyo wa zamani wa Zanzibar alikuwa akitoa maoni
yake baada ya kuombwa na gazeti hili kutoa tathmini yake ya mwaka 2017.
Alisema viongozi wa dini wamehisi kuna kasoro fulani ndani ya
Serikali ndiyo maana wamesema hayo na kwamba, si jambo jipya kutokea kwa
kuwa walishawahi kukosoa Serikali zilizopita.
Alisema wakati wa utawala wa Mwinyi na Kikwete, kulikuwa na barua
za kichungaji za kuisema na kuikosoa Serikali, lakini marais hao wote
walikuwa wavumilivu na walisikiliza maoni yao.
“Yale yanayofurahisha yachukuliwe na yale yanayokera
vumilia. Kisha uyachukue na ujiulize hivi ni kweli aliyoyasema baba
askofu au ameweka chumvi?” alisema Maalim Seif ambaye amewahi pia kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Alibainisha kuwa kiongozi anatakiwa kusikiliza zaidi kauli za
kumkosoa ili azifanyie kazi huku akitahadharisha kwamba kuna watu kazi
yao ni kusifia viongozi hata katika jambo lisilo na msingi na kuonya
kuwa hao ni hatari zaidi.
“Kauli za kukosoa azifanyie kazi kuliko za kumsifia.
Lazima atambue kuwa kuna watu wanajipendekeza kwa kusifia viongozi na
kuwapandisha chati hadi mbinguni kwa sababu ya masilahi yao,” alisema.
“Umakini unahitajika hapa, hasa kwa watu wanaopenda
kusifusifu kwa kila jambo. Wale wanaokosoa ndiyo wasikilizwe zaidi.
Utawala wa Magufuli una mazuri na wanasiasa wasione tabu kuyasema na
watawala wasione aibu kukoselewa, bali wavumilie.
“Marehemu Spika wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta, aliwahi kusema mwanasiasa lazima uwe na ngozi ngumu ya kuvumilia.”
Maalim Seif pia alimpongeza Rais Magufuli kwamba amejitahidi
kudhibiti utoroshwaji wa madini na kuhakikisha rasilimali hizo
zinawanufaisha Watanzania.
“Amepambana na rushwa kwa sasa imepungua. Amerejesha
nidhamu serikalini. Kwa sasa si rahisi kukuta rushwa, ingawa bado kuna
maeneo ipo. Awamu hii imejitahidi kupambana na mapapa wa rushwa na si
vidagaa,” alisema.
Kuhusu takwimu za uchumi kuonekana kukua huku wananchi wakidai fedha zimepungua mifukoni, alisema: “Mwaka
2017 wananchi wengi walikuwa na matumaini makubwa ya kuwa na maisha
mazuri, lakini imekuwa kinyume. Hali ni ngumu. Ugumu wa maisha si Bara
tu hata huku Zanzibar.
“Pale Dar es Salaam baadhi ya wafanyabiashara wamefunga
maduka yao. Ingawa Serikali kwa nyakati tofauti inasema uchumi unakua,
lakini si kweli. Tunataka hali ya uchumi iendane na hali halisi ya
maisha ya wananchi. Takwimu za kwenye makaratasi hazitasaidia.”
Kuhusu demokrasia, Maalim Seif alisema kwa sasa imerudi nyuma hasa
baada ya Rais Magufuli kupiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano
licha ya kuwa mambo hayo yapo kwa mujibu wa sheria. “Kupiga
marufuku mikutano ya hadhara kumeathiri utendaji kazi wa vyama vya
siasa. Kazi ya chama cha siasa ni kuwatafuta wanachama ambao
hawapatikani kama vyama havielezi sera na mikakati yao. Usipopata nafasi
hiyo huwezi kufanikiwa,” alisema.
Chanzo-Mwananchi na zanzibar24.
Comments