Leo ni siku ya Jumatatu 15 Januari, 2018.

Jumatatu 15 Januari, 2018Leo ni Jumatatu tarehe 27 Rabiuthani 1439 Hijria sawa na Januari 15, 2018.

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita inayosadifiana na tarehe 25 Dey 1357 Hijria Shamsia, kulitokea mapigano makali baina ya jeshi la utawala wa Shah na wananchi wa Iran kufuatia maandamano ya mara kwa mara ya wananchi dhidi utawala huo wa kidikteta. 
Katika mapigano hayo baadhi ya wanajeshi waliotambua sababu za mapambano ya wananchi, waliamua kuzikimbia kambi zao za kijeshi na kujiunga katika safu za wananchi. 
Kujiunga wanajeshi na safu za wananchi ilikuwa bishara njema ya mabadiliko makubwa katika moyo na muundo wa jeshi la utawala wa Shah.
Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kishia. Akiwa na miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini. 
Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari alielekea mjini Arak, Iran katika kipindi cha kuasisiwa chuo cha hauza cha mji huo na kujishughulisha na ukufunzi. 
Baadaye msomi huyo alishirikiana na Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi katika shughuli za tablighi na baada ya kuasisiwa hauza ya Qum, chini ya usimamizi wa Ayatullah Hairi Yazdi, Ayatullah Ahmad Khansari alikuwa imamu wa swala ya jamaa katika chuo cha Faiziya mjini humo. 
Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Tehran na kuwa imamu wa Swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. 
Hadi mwisho wa uhai wake msomi huyo alisalia mjini Tehran na baada ya kufariki dunia akazikwa mjini Qum.
Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari
Na siku kama ya leo miaka 179 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 15 Januari 1839, nchi ya El Salvador ilijitangazia rasmi uhuru wake baada ya kusambaratika Muungano wa Amerika ya Kati. El Salvador ambayo ilikuwa ikikoloniwa na Uhispania kwa miaka kadhaa, ilipatia uhuru mwaka 1821. Nchi hiyo ilikabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi mwaka 1931, baada ya kuporomoka bei ya kahawa katika soko la dunia, zao lililokuwa likitegemewa nchini humo. Hali mbaya ya kiuchumi iliwakasirisha wananchi wa nchi hiyo, na kuzusha uasi wa wananchi na wanachuo dhidi ya dikteta Jenerali Maximiliano Hernandez Martinez wa El Salvador.
Bendera ya El Salvador
 sehemu hii imeletwa kwenu kwa udhamin na parstoday.

Comments