Leo ni siku ya Jumatano, Januari 31, 2018.

Jumatano, Januari 31, 2018Leo ni Jumatano tarehe 13 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1437 Hijria sawa na Januari 31, 2018 Milaadia.

Siku kama ya leo miaka 1428 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia, Bibi Fatma Zahra binti wa Mtume Muhammad SAW alikufa shahidi baada ya kuishi maisha mafupi lakini yaliyojaa baraka tele. Baba yake ni Mtume Muhammad SAW na mama yake ni Bibi Khadija binti Khuwaylid AS. 
Bibi Fatma alishiriki katika medani mbalimbali za kipindi cha mwanzo mwa Uislamu akiwa bega kwa bega na Mtume wa Mwenyezi Mungu, Imam Ali bin Abi Talib AS na Waisalmu wengine walisabilia nafsi zao kwa ajili ya dini hiyo ya Mwenyezi Mungu na alilea watoto wema, kama Imam Hassan na Hussein AS ambao Mtume (saw) amesema kuwa ni viongozi wa mabarobaro wa peponi. 
Bibi Fatma alisifika mno kwa tabia njema, uchaji Mungu na elimu na alikuwa mfano na kigezo chema cha Waislamu.
Siku kama ya leo miaka 419 iliyopita, ilianzishwa kampuni ya kwanza ya Uingereza ya India Mashariki nchini India, kwa amri ya Malkia Elizabeth wa Kwanza wa Uingereza. 
Kampuni hiyo, iliimarisha ukoloni wa Uingereza katika maeneo yenye utajiri, huko kusini mwa Asia na baada ya hapo shughuli za ukoloni na mahusiano ya kisatwa ya London yakaimarika kupitia kampuni hiyo. 
Baada ya kuasisiwa kampuni hiyo, nchi nyingine kama vile Uholanzi, Ureno na Ufaransa zikaelekeza nguvu zao barani India kwa lengo la kuhudumia ukoloni wao. 
Aidha baada ya karne 3 za kuanzishwa shirika hilo, satwa na kuimarika utawala wa Uingereza nchini India vilisababisha nchi hiyo kutangazwa kuwa sehemu ya Uingereza na Malkia Viktoria akavikwa taji la kuwa mtawala wa India na Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 168 iliyopita, ilianzishwa harakati kubwa ya wananchi wa China iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Taiping. 
Harakati hiyo ilitokana na hali mbaya na umasikini uliokuwa ukiwasumbua wananchi wa nchi hiyo na hasa matabaka ya watu wa vijijini, iliyosababishwa na ukoloni wa kigeni na utawala wa familia isiyofaa ya Manchu. 
Lengo kuu la harakati hiyo iliyodumu kwa muda wa miaka 14 lilikuwa ni kuwepo usawa katika kugawana ardhi kati ya wanawake na wanaume.
Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita gwaride la mwisho na kimaonyesho la vikosi vya majeshi ya utawala wa Shah lililokuwa na lengo la kuwatia hofu na woga wananchi Waislamu wa Iran, lilifanyika katika mitaa mbalimbali ya Tehran. 
Katika gwaride hilo, wanajeshi wengi walionesha mshikamano wao na kuungana na wananchi Waislamu wa Iran na kuamua kuanza mapambano dhidi ya utawala wa kibeberu wa Shah.
 hii nikwa hisani ya parstoday.

Comments