leo ni siku ya Jumanne Januari 16, 2018

Leo ni Jumanne tarehe 28 Jamadithani 1439 Hijria sawa na Januari 16, 2018.


Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita Muhammad Ridha Pahlavi mfalme wa mwisho wa Iran alikimbia nchi kwa kisingizio cha matibabu baada ya kupamba moto mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran. 

Mwaka 1320 Hijria Shamsiya Muhammad Ridha Pahlavi alikalia kiti cha usultani baada ya serikali ya Uingereza kumbaidisha baba yake Ridha Shah kutokana na hatua yake ya kuiunga mkono Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. 

Mwaka 1332 Hijria Shamsiya Shah kwa mara nyingine tena aliikimbia Iran kufuatia mapambano ya wananchi, hata hivyo siku tatu baadaye yaani tarehe 28 mwezi Mordad, Shah alirejea nchini baada ya mapinduzi yaliyoendeshwa na Marekani na Uingereza dhidi ya wananchi wa Iran.
 
Miaka miaka 61 iliyopita katika siku sawa na ya leo alifariki dunia mtunzi wa nyimbo mwenye asili ya Italia kwa jina la Arturo Toscanini. 

Toscanini alizaliwa mwaka 1867 na alianza kupenda muziki akiwa kijana. Arturo Toscanini alikuwa kiongozi wa bendi baada ya kufanya mazoezi mengi na kusafiri katika nchi mbalimbali duniani. 

Aidha alipata umashuhuri kutokana uwezo wake mkubwa wa kuhifadhi na kuwa makini katika utunzi wa nyimbo. Toscanini aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 90 yaani miaka mitatu baada ya kustaafu kazi ya muziki.
Miaka 172 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo vita kati ya Marekani na Mexico vilianza kufuatia uvamizi uliofanywa na Marekani dhidi ya nchi hiyo. 

Marekani ilianzisha vita hivyo vilivyodumu kwa miaka miwili dhidi ya Mexico kwa kisingizio kwamba wahamiaji wa Marekani walikuwa wakisumbuliwa huko Mexico, lakini ukweli ni kuwa Marekani ilikuwa ikikusudia kuyaunganisha baadhi ya maeneo ya Mexico na ardhi yake khususan jimbo la Texas.
Na miaka 801 iliyopita katika siku sawa na ya leo Abubakar Muhyiddin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Arabi, arif na msomi mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia huko Damascus. Alizaliwa mwaka 560 Hijria huko Andalusia, Uhispania ya leo. 

Ibn Arabi alifanya safari nyingi katika baadhi ya nchi na miji ikiwemo Tunisia, Makka na Baghdad na kila alipofika aliheshimiwa na kukirimiwa. 

Alikuwa msomi hodari na baadhi ya duru zinasema kuwa ameandika vitabu na risala zaidi ya 500. 

Miongoni mwa kazi zake kubwa ni vitabu vya "Tafsir Kabir", "al Futuhatul Makkiyyah" na "Fususul Hikam".
 chanzo:parstoday.

Comments