KIKOSI
cha Mbao FC, huenda kimewashangaza wengi kutokana na hatua kubwa
kinachozipiga ikiwa ni siku chache baada ya kubomolewa na klabu kubwa za
soka nchini.
Baada
ya msimu wa 2016-17 kwisha, Mbao FC ilibomolewa baada ya wachezaji wake
kwenda katika klabu kubwa za Yanga, Simba na Azam FC kwa ajili ya msimu
wa 2017-18.
Kuondoka
kwa wachezaji hao kulizua hisia za hofu kwamba huenda mwisho wa Mbao FC
kufanya vema na kuwa tishio kwa vigogo ulikuwa ndiyo kuwadia.
Wengi
waliona Mbao FC walikuwa wamekosea na huenda hata taarifa kuwa kocha
wake, Etienne Ndayiragije kuwa alikuwa anatarajia kuondoka zilifanana
sana na zile hisia za mashabiki kwamba huenda kocha huyo hakufurahia
kuuzwa kwa nyota wake mfululizo.
Lakini
baadaye kocha huyo raia wa Burundi aliendelea kubaki katika kikosi cha
Mbao FC hadi sasa. Lakini kilichovutia zaidi ni namna alivyoweza
kuijenga upya timu yake ikiwa bila ya wachezaji waliotegemewa msimu
mmoja uliopita.
Utakuwa
unakumbuka, kwamba kikosi hicho, msimu uliopita, kiliwavua Yanga
ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports ikiwa ni pamoja na
kuwaangusha kwa kipigo.
Lakini
walipotinga fainali ya Kombe la Shirikisho ya Simba, pale Uwanja wa
Jamhuri mjini Dodoma kulichimbika kwelikweli na Simba waliuchukua
ubingwa ule wakilala na viatu.
Msimu
huu, Simba wamekutana na Mbao FC katika Ligi Kuu Bara, mechi hiyo
kwenye Uwanja wa CCM Kirumba iliisha kwa sare ya mabao 2-2, Mbao FC
wakisawazisha mara zote.
Mechi
nyingine na kigogo, ilikuwa dhidi ya Yanga juzi hapohapo CCM Kirumba,
Yanga wamekubali kipigo cha mabao 2-0, hiki kikiwa cha pili mfululizo.
Wakati
Mbao FC wanakutana na Yanga, kuna kitu unaweza kujifunza. Kwamba
wanacheza kwa kujiamini, wanaonyesha soka safi lakini wanafunga mabao
mazuri kabisa, kama ambayo walifunga dhidi ya Simba.
Mechi
mbili dhidi ya Yanga na Simba, Mbao FC wamefunga mabao manne na
wamefungwa mawili tu. Hii si timu ya kubeza na Ndayiragije, si mtu wa
kumbeza tu.
Tokea
mwanzo, nimezungumzia timu na baadaye nimegusa kuhusiana na wachezaji
wanavyokuwa wanacheza wakijiamini na zaidi ningependa kumzungumzia
mshambuliaji wa Mbao FC, Habibu Haji Kiyombo.
Kiyombo
amefunga mabao matatu ya Mbao FC dhidi ya Yanga na Simba. Alifunga moja
mechi ya 2-2 dhidi ya Simba lakini akarudia na kufunga mawili Yanga
ilipolala 2-0.
Wakati
Kiyombo anafunga mabao hayo, utaona huwezi kuona hata mshambuliaji
mmoja wa Simba au Yanga mwenye mawili, au huwezi kuona washambuliaji wa
kimataifa wa timu hizo kuwa walifanya vema dhidi ya Mbao FC.
Hiyo
haitoshi, Kiyombo amefunga mabao matatu dhidi ya Yanga na Simba katika
mechi hizo mbili. Lakini mabao yake mawili yanafanana kabisa na unaweza
yote mawili ukayaingiza kwenye shindano la bao bora Ligi Kuu Bara.
Dhidi
ya Simba, Kiyombo alimtoka beki mmoja, akiwa umbali wa takribani mita
25 hadi 28, akaachia mkwaju mkali uliomshinda Aishi Manula na kuandika
bao la kwanza la Mbao FC.
Mechi
dhidi ya Yanga, Kiyombo alirudia, safari hii akiwatoka mabeki wawili wa
Yanga na kuachia mkwaju wa chinichini uliojaa moja kwa moja wavuni na
kuandika bao la kwanza la Mbao FC dhidi ya Yanga kabla ya kuongeza la
pili.
Unaweza
kujiuliza, kijana huyu anapata wapi hali ya kujiamini na kufunga mabao
matatu dhidi ya Yanga na Simba lakini mabao bora kabisa ambayo wakati
mwingine ni vigumu kuona washambulizi wa kimataifa wanaocheza hapa
nyumbani wakifunga mabao kama hayo!
Alijiamini nini au ana nini ambacho huenda hatujakiona na huenda ni nafasi nyingine ya kuanza kukitambua na kukifanyia kazi?.
Tena
kwa mabao hayo matatu ya Yanga na Simba, maana yake yeye ndiye mchezaji
aliyefunga mabao mengi zaidi dhidi ya watani wa jadi kwa msimu huu wa
2017-18 na inawezekana ndiye mchezaji hadi sasa amewafunga wakongwe hao
mabao mazuri zaidi.
Tukubaliane,
Kiyombo ana kitu ambacho sasa kinapaswa kutazamwa na ikiwezekana apate
nafasi zaidi. Sisemi hivi nimvimbishe kichwa, badala yake naona ana kitu
kinachoweza kumpeleka mbali zaidi.
Kama
ingekuwa ni uwezo wangu na ndiye mtu wa mwisho kuamua ningesema huenda
vizuri asiende Yanga wala Simba na apitilize tu kama ilivyokuwa kwa
Thomas Ulimwengu.
Mbwana
Samatta alikaa kidogo Simba, ikampa nafasi ya kusonga. Lakini ninaamini
Kiyombo akipata timu kubwa ya nje, ana nafasi kubwa ya kufanya vizuri
kwa kuwa ana kipaji, ana nia na asiye na hofu ya kufanya utekelezaji.
Kikubwa
kabisa kwa Kiyombo anachotakiwa ni kukiendeleza kipaji chake kwa
kujifunza na awe makini asivimbe kichwa lakini pia asisikilize miluzi
mingi.
Comments