Kamati ya uendeshaji na usimamizi ya Bodi ya Ligi
imewachukulia hatua waamuzi wote waliochezesha mchezo wa ligi daraja la
kwanza kati ya Dodoma FC dhidi ya Alliance uliopigwa mjini Dodoma
Jumamosi iliyopita ambapo mwamuzi wa kati alikuwa ni Andrew Shamba
ambaye alionekana kuboronga zaidi katika mchezo huo na kuchezesha chini
ya kiwango.
Kitu ambacho kilistua wengi ni mwamuzi huyo kutoa kadi nne nyekundu kwa timu mmoja (Alliance)
Afisa mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi Boniface Wambura amethibitisha:
“Katika mechi hiyo, waamuzi wote wanne wamefungiwa miaka mitatu kila
mmoja na sababu ya kuwafungia ni kwamba walichezesha mechi chini ya
kiwango.”
“Ripoti ya kamishna imeonesha hivyo na adhabu yao imezingatia kanuni
ya ligi daraja la kwanza inayohusu udhibiti wa waamuzi na ikumbukwe kati
ya waamuzi hao wawili ni waamuzi wa ligi kuu Tanzania bara kwa hiyo
kamati imeona kwamba kama mwamuzi wa ligi kuu anakwenda kuchezesha mechi
ya daraja la kwanza chini ya kiwango kamati iliamini kamati ya waamuzi
iliwapa mechi hiyo wakiamini wataiendesha vizuri.”
“Kamati ilitafakari sana hicho kiwango kilichooneshwa na waamuzi na
haikuridhika hivyo imeona kwamba inawezekana kuna ushawishi mwingine
uliwafanya waamuzi hao wachezeshe kwa kiwango hicho.”
“Kamati imewasiliana na TFF ikiomba suala hili liende kwenye vyombo
vingine vya uchunguzi vinavyohusiana na makosa mengine ya rushwa kwa
sababu TFF haina mamlaka au vyombo vinavyoweza kuchunguza masuala ya
rushwa, tunashukuru TFF wameshapeleka barua TAKUKURU na sisis tumepewa
nakala.”
Kamishna wa mchezo huo pia hakuna, amefungiwa miaka mitatu kwa
kushindwa kutoa taarifa yenye usahihi kwa sababu kamati imeangalia
taarifa na kugundua haikujitosheleza kuonesha nini hasa kilitokea wakati
wa mechi.
Comments