
Akiwa katika eneo hilo lililoko Mangapwani-Bumbwini lenye ukubwa wa
hekta 399.25 sawa na hekari 986.5, Rais Dk. Shein aliyeongozana na
viongozi mbali mbali wa Serikali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Balozi
Seif Ali Idd, Mawaziri na viongozi wengine wa Serikali, wakiwemo wajumbe
wa Baraza la Mapinduzi, alipata maelezo kuhusu hatua zinazoendelea
katika mradi huo.
Kwa maelezo ya Katibu wa Kamisheni ya Ardhi Ahmed Abdulrahman Rashid
alimueleza Dk. Shein kuwa eneo hilo lenye ukubwa wa hekta hizo tayari
limetengwa kwa ajili ya shughuli zote za mafuta na gesi asilia, bandari
pamoja na bohari kuu ya Serikali ya kuhifadhia mafuta.
Aidha, alimueleza Rais Dk. Shein kuwa azma ya mradi huo ni kwamba
baada ya kukamilika shughuli zote za mafuta zinazofanywa katika bohari
ya Mtoni zitahamishwa na kuhamia katika eneo hilo maalum lililolengwa na
Serikali.
Kwa mujibu wa maelezo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Maji,
Nishati na Mazingira Ali Halil Mirza, hatua inayoendelea hivi sasa ni
kufanywa kwa uchambuzi yakinifu unaotekelezwa na Benki ya Dunia ambao
utakamilika kwa muda wa miezi sita ijayo.
Mirza alieleza kuwa kukamilika kwa uchambuzi huo yakinifu ndio
utaleta mapendekezo ya kulisanifu eneo hilo kwa ajili ya bandari na
majengo mengine ya utawala na shughuli nyengine zinazoenda sambamba na
mradi huo.
Kwa mujibu wa maelezo ya viongozi wa Wizara hiyo, miongoni mwa sababu
ya kutengwa eneo hilo kwa shughuli hizo ni kutokana na kuwa na kina
kirefu cha maji ya bahari ambacho kitarahisisha kujengwa kwa bandari
hiyo muhimu ambayo itatumika kwa ajili ya kusafirishia gesi asilia na
mafuta ndani na nje ya nchi.
Uongozi wa Wizara hiyo, ulieleza kuwa miongoni mwa faida kubwa za
mradi huo mara baada ya kukamilika kwake ni pamoja na kuondoa kabisa
uhaba wa mafuta hapa nchini sambamba na kuweza kuuza hata nje ya nchi na
kuipatia Serikali pato kubwa.
Sambamba na hayo, uongozi huo wa Wizara hiyo ulieleza kuwa Mradi huo
ambao utakuwa na bandari, matangi ya mafuta kwa kuwa na sehemu ya bohari
ya Taifa ya kuhifadhia gesi asilia na mafuta ni hatua za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha sekta ya nishati hapa nchini.
Wakati huo huo, Dk. Shein akiwa na ujumbe wake alipata fursa ya
kulikagua eneo la Kampuni ya Salama International Trading Co Ltd,
linalojengwa maalum kwa ajili ya kusafisha mafuta na kupata maelezo
kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Abdalla Said Abdalla na kumueleza
hatua zilizofikiwa na Kampuni yake katika ujenzi huo.
Kwa maelezo ya Mkurugenzi huyo, alisema kuwa eneo hilo ambalo ni kwa
ajili ya kusafisha mafuta ambalo limefikia asilimia 65 za ujenzi, lina
lengo la kujenga jeti kwa ajili ya kushushia mafuta na kutia kwenye
matangi yaliopo katika eneo hilo.
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa Matenki tani elfu 18, sawa na lita
milioni 24 ambayo yanaweza kuhifadhiwa kwa wakati mmoja, huku akieleza
aina za mafuta yatakayohifadhiwa katika matenki hayo yakiwemo mafuta ya
diseli, petroli na mafuta ya taa pamoja na mafuta ya kulainisha mitambo
huku.
Uongozi huo ulieleza kuwa tayari wanabaraka zote kutoka Serikalini
ikiwemo kutoka kwa Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), na kutoa
shukurani kwa Serikali kupitia Idara zake zote ikiwemo Mazingira, Ardhi
pamoja na (ZIPA) na kutoa shukurani kwa Rais Dk. Shein kwa ziara yake
hiyo.
Walieleza kuwa kuanzia Februari mwaka huu wataendelea na shughuli za
ujenzi zilizobaki shughuli ambazo ziliaza mwaka 2015 kwa awamu tatu
ambapo hadi walipofikia washatumia dola milioni 5 kwa awamu ya kwanza na
kueleza kuwa watazalisha tani 600 ambazo zitawasidia Wazanzibari
wenyewe kwa asilimia 70 na asiliamia zilizobaki watauza nje ya nchi.
Walieleza kuwa Watu wa Bandari, Uhamiaji na Idara zote muhimu
zitakuwepo katika eneo hilo ambalo tayari wameshaanza ujenzi wa jengo
maalum kwa wahusika hao.
Akiwa katika eneo hilo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya uhifadhi
wa mazingira katika mchakato wa usafishaji wa mafuta mara
utakapokamilika mradi huo ambapo Mkurugenzi wa Kampuni hiyo alimtoa wasi
wasi na kumueleza kuwa aina ya mafuta wanayokusudia kusafisha haitakuwa
na athari zitakazopelekea uharibifu wa mazingira kutokana na aina hiyo
ya mafuta ambayo watachukua kutoa nchini Oman na Iran.
Pia, Dk. Shein alitembelea eneo la Kampuni ya Turkey Petrolium (TP),
ambalo limetengwa kwa ajili ya gesi na mafuta ambapo uongozi wa Kampuni
hiyo ulieleza kuwa juhudi za makusudi wanazichukuwa katika kuhakikisha
Zanzibar inafaidika kwa gesi mara baada ya kujengwa kwa Chelezo ambapo
meli maalum zitaleta gesi moja kwa moja kuanzia mwezi wa sita hapa
Zanzibar.
Aidha, uongozi huo ulieleza azma ya kujenga jengo maalum ambalo
litasaidia kwa ajili ya kuwaweka wafanyakazi wa Kampuni yao pamoja na
Idara nyengine muhimu zinazohusiana na shughuli hizo zikiwemo Uhamiaji
na nyenginezo.
Pamoja na hayo, uongozi huo uliiomba Serikali kuwezesha azma yao hiyo
kutokana na baadhi ya changamoto zilizopo hivi sasa ikiwemo uhaba wa
gesi mara kwa mara kutokana na sehemu wanayochukulia gesi hiyo.
Uongozi wa Kampuni hiyo ya Turkey Petrolium (TP), ulieleza kuwa
mashirikiano mazuri yamekuwepo kati yao na Mamlaka ya Uwekezaji Vitega
Uchumi Zanzibar (ZIPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Maji na Nishati
Zanzibar (ZURA), Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Ardhi, Maji,
Nishati na Mazingira Wizara ya Biashara.
Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa wanunuzi wakuu wa gesi katika
Kampuni yao hiyo kwa hivi sasa ni wananchi pamoja na hoteli huku uongozi
huo ukisisitiza kuwa kuwepo kwa chelezo kwa ajili ya kuingizia meli
ambazo zitaleta gesi moja kwa moja kutawarahisishia zaidi uendeshaji wa
mradi wao huo.
Nae Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Maji na Nishati
Zanzibar (ZURA), Haji Kali Haji alieleza mashirikiano yaliopo kati ya
Mamlaka yake pamoja na Kampuni hiyo ambapo mapema alieleza mashirikiano
na hatua zinazochukuliwa katika kuhakikisha eneo maalum lilotengwa na
Serikali kwa ajili ya shughuli za mafuta na gesi asilia linafikia na
malengo yaliokusudiwa na Serikali.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
chanzo: Zanzibar24
Comments