Azam hii weka mbali na watoto.

MABINGWA watetezi wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC wameendeleza makali yao kwenye mashindano ya msimu huu baada ya kushinda mechi mbili mfululizo tena bila kuruhusu bao.
Azam ilitwaa taji hilo mwaka jana kwa rekodi kucheza michezo yote sita bila kuruhusu bao lolote katika wavu wao jambo ambalo wameanza kulirudia msimu huu kwani katika mechi zao mbili hawajaruhusu bao.
Matajiri hao wa Ligi Kuu Bara wamezifunga Mwenge mabao 2-0, na Jamuhuri 4-0.
Azam pia ina rekodi ya kutokufungwa mchezo wowote katika mechi nane za mashindano hayo tangu msimu uliopita. Mwaka jana ilicheza mechi sita bila kupoteza.
Kocha Msaidizi wa Azam FC, Iddi Cheche alisema usajili na mabadiliko waliyoyafanya katika dirisha dogo yameongeza marali katika kikosi chao hasa katika safu ya ushambuliaji ambayo ilikuwa haifungi zaidi ya bao moja.
“Tuna vijana wengi katika timu yetu. Wengi wao ndio mara ya kwanza wanacheza Ligi Kuu na mashindano kama haya,” alisema Cheche ambaye alikuwa mchezaji wa zamani wa Sigara ya jijini Dar es Salaam.
“Kuimarika kwa viwango vya wachezaji kama Salim Hoza kumeongeza kasi na uimara wa timu yetu ndio maana tumeaanza kula matunda kwa kupata matokeo na mabao mengi tofauti na hapo awali,” aliongeza kocha huyo. 

Comments