Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema wakati umefika kwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutowapa nafasi za uongozi wenye tabia ya kuhama majimbo.
Balozi Iddi alisema hayo jana wakati ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa Magharibi wa kuwachagua viongozi watakaouongoza mkoa huo kwa kusaidiana na viongozi wengine katika kipindi cha miaka mitano ijayo 2017–2022.
Alisema wanachama hao huyakimbia majimbo yao ya zamani na kutaka kuhamia mapya baada ya kujibaini kutowatumikia vyema wapigakura katika nafasi za ubunge na uwakilishi.
Balozi Iddi alisema sifa ya wanachama lazima iende sambamba na uwezo wa kiongozi kwa kuwashawishi wasiokuwa wanachama kujiunga CCM.
Alisema wanachama wanapaswa kuzingatia mwelekeo wa viongozi wa chama chao.
Balozi Idd alitahadharisha kuwa utegemezi siku zote unawajengea nguvu wale wanaowategemea.
Alitoa wito kwa uongozi utakaochaguliwa kuwa utakuwa na jukumu la kusimamia na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015–2020.
Aliwapongeza viongozi wa Mkoa Magharibi kwa kutekeleza Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la 2017 Ibara ya 87 (4) kwa kufanya uchaguzi wa viongozi mkoa.
Katibu wa CCM wa mkoa huo, Aziza Ramadhan Mapuri alisema chama hicho kimepata mafanikio katika kujenga upendo miongoni mwa wanachama.
Alisema upendo huo umeuwezesha uongozi wa mkoa kuisimamia vyema Serikali katika utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi aliyemaliza muda wake, Yussuf Mohamed Yussuf alisema kwamba chaguzi zilizokuwa zikiendelea ndani ya chama kuanzia ngazi ya shina hadi mkoa ni matukio muhimu ya kuendeleza demokrasia ndani ya chama.
chanzo:Mwananchi.
Comments