Wakazi wa Kimara wakwepa kupanda daraja.

Kwa muda sasa, wakazi wa wanaotumia Barabara ya Morogoro hasa maeneo ya Kimara na Mbezi wamekuwa wakikabiliwa na foleni.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kiini cha foleni hiyo ni msongamano wa watu, pikipiki, bajaji na magari katika kituo cha Kimara Korogwe.
Msongamano huo unachangiwa kwa kiasi kikubwa na abiria wanaokwepa kushuka Kimara Mwisho kwa kukwepa kupanda daraja ambalo ndilo linalotumika kama kivuko.
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo waliohojiwa akiwamo, Nusura Said wamesema hatua hiyo ndicho chanzo kikubwa cha foleni kwa kuwa magari yanalazimika kusimama kuwapisha wanaovuka.
Alisema wakazi wa Kimara na Mbezi wanaotoka na kwenda mjini hushukia Korogwe kwa ajili ya kupata usafiri wa kuunganisha.
“Watu wanashuka na mwendo kasi kutokea mjini wanatembea au kupanda bodaboda kwenda Kimara Mwisho, hata wale wanaotokea Mbezi, Kibamba wanashuka hapa na kuunganisha magari ya kwenda mjini hilo linasababisha muda wote kuwe na msongamano wa watu.
“Mtu anaona kutumia dakika tano au sita kupanda daraja ni mtihani mkubwa hivyo bora ashuke hapa akatishe au apande usafiri mwingine,”
Kauli hiyo iliungwa mkono na dereva wa bodaboda, Thomas Mangi, “Utakuta watu wanavuka ovyo ovyo wakati mwingine bila kujali magari, hali hiyo inasababisha usumbufu kwa madereva.
Wingi huo wa abiria umevivutia vyombo vya usafiri; daladala, bajaji na pikipiki na kuhusu hilo, Amani Lazaro ameelekeza lawama kwa madereva wa daladala, “Sioni kama watu wanaovuka wana athari zozote, msongamano unasababishwa na hizi daladala, wanaacha kituo chao wanageuza hapa wakiamini ndiyo kuna abiria wengi.”
Wakati wengi wakiamini kuwa watu wanakwepa kupanda daraja kwa sababu ya uvivu, mwanasaikolojia Modesta Kamonga alikuwa na mtazamo tofauti, alisema hali hiyo inachangiwa na woga ambao kwa kitaalamu ni ugonjwa unafahamika kama “Forbia”.
“Kisaikolojia mtu kuhofia kupanda daraja ni woga, mtu anakuwa na wasiwasi kuwa huenda akipanda ataanguka au atasikia kizunguzungu lakini haina uhusiano wowote na uvivu,” alisema.
Kuhusu daraja hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Ronald Rwakatare alisema muundo wake umesanifiwa kuwawezesha pia watu wenye ulemavu kulitumia.
Alisema kabla ya mradi, waliwashirikisha wadau wote lakini sasa wakati wa utekelezaji wanakabiliana na changamoto ya watu kutolitumia badala yake wengi wanakitumia kituo cha Kimara Korogwe.
chanzo:Mwananchi.

Comments