Urejeshaji fomu za maadili wagubikwa na mkanganyiko.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na
Wakati urejeshaji wa fomu za tamko la rasilimali na madeni kwa viongozi wa umma ukifikia tamati leo, imebainika kuwa baadhi wamejikanganya kwa kuzipeleka bila kujaza licha ya kuwa na mhuri wa hakimu.
Miongoni mwa watumishi waliorudisha fomu hizo bila kuzijaza ni wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.
Akizungumza ofisini kwake jijini Mbeya jana, mkuu wa Sekretarieti ya Maadili kwa Viongozi wa Umma Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Erick Mbembati alisema baadhi ya viongozi wamezirejesha zikiwa na kasoro nyingi, hivyo hazikupokewa.
Mbembati alisema moja ya kasoro walizobaini ni kutojazwa huku zikiwa zimegongwa mhuri wa hakimu.
Alisema katika fomu nyingine taarifa zimejazwa nusunusu na wengine wamejaza vizuri, lakini hazikupelekwa kwa kamishna wa kiapo hivyo walikuwa wakiwarudisha kwenda kurekebisha kabla ya kupokewa.
“Kwa mfano, jana kuna kiongozi tena mkubwa tu, ameleta fomu yake imegongwa mhuri wa hakimu lakini ndani haijajazwa kitu chochote, hii inaonyesha hata hakimu amethibitisha kitu bila kujiridhisha kwanza.
“Na sitaki kuamini eti hakimu au wakili hajui kitu hadi anafikia uamuzi wa kugonga mhuri kwa kitu asichokishuhudia.
“Hii ni hatari sana na niwakumbushe mahakimu na mawakili kwamba wajibu wao siyo kugonga mhuri pekee, bali ni pamoja kusimamia kiapo kwa kuangalia taarifa za mteja wako kikamilifu. Najiuliza hakimu unawezaje kusimamia kitu kisichokuwepo?” alihoji Mbembati.
Alifafanua kuwa kitendo hicho kinawapotezea rasilimali muda wahusika na usumbufu wa kurudi mara mbili katika ofisi hizo kwa kuwa hawezi kukubali kupokea fomu ya kiongozi ikiwa na taarifa zenye makosa.
“Haya yote ni madhara ya kufanya jambo dakika za mwisho, mtu unakuwa na haraka zako, hivyo unafanya kazi kwa kulipua lipua tu.
“Walikuwa na muda mzuri wa kutekeleza hili kuanzia Desemba Mosi hadi 31. Sasa hebu piga hesabu mtu ametoka Njombe, Songwe, Rukwa huko halafu anafika hapa fomu yake inakataliwa na mbaya zaidi awe ameagiza mtu amletee,” alisema.
Ikiwa leo ni mwisho, Kamishna wa Maadili wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji mstaafu Harold Nsekela alisema ofisi zitakuwa wazi ili kuruhusu watumishi na viongozi wa umma kurudisha fomu.
Jaji Nsekela alisema ofisi zitafunguliwa ili kuepuka maneno ya watu watakaoshindwa kurejesha fomu hizo.
“Tutafungua kama kawaida saa za kazi, hatutaki maneno na viongozi wasije kusema kama mwisho Desemba 31 ni kwa nini ofisi zisifunguliwe, sasa tunawaambia waje,” alisema Jaji Nsekela.
Alifafanua kuwa Jumanne wataanza kuzipitia na kama watakuwapo ambao hawakuzirejesha, baada ya uchambuzi ataeleza.
Tofauti na ilivyokuwa juzi, ni watumishi wachache waliojitokeza jana jijini Dar es Salaam.
Huko Mbeya, Diwani wa Forest, Henry Mwangambaku alisema changamoto ni nyingi zinazofanya wengi washindwe kurudisha fomu kwa wakati.
“Huu ni utaratibu wa kila mwaka, siyo kwamba leo watu wamemiminika ofisini hapa kwa vile kuna tamko, hapana! Kuna changamoto nyingi.
“Kwanza hizi fomu zinapatikana kwenye mtandao, hivyo ukiachana na sisi tunaoishi mijini, wale wanaotoka vijijini huko ambako jiografia yake ni ngumu wapi atapa kupakua (download) fomu hizi?” alihoji Mwangambaku.
Alifafanua kuwa hata ofisi hizo hazipo kila wilaya, bali ni Mbeya Mjini kwa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, hivyo viongozi wanaotoka mbali inakuwa vigumu kuendana na muda kwa kuwa hata akipakua mtandaoni kuna mchakato wa kuwatafuta mawakili au hakimu wa kuthibitisha taarifa kabla ya kurejesha.
chanzo:Mwananchi.

Comments