Uhaba wa Vyoo: Walimu na Wanafunzi Foleni kwenda kujisaidia.

Wanafunzi na Walimu katika Shule ya Msingi Halawa, iliyopo wilayani Bariadi mkoani Simiyu, wanakabiliwa na ukosefu wa matundu ya vyoo hali inayowalazimu kujisaidia kwa zamu kwenye choo kimoja.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Masota Masota amesema shule yao inakabiliwa na changamoto nyingi za miundombinu, ikiwamo hiyo ya ukosefu wa matundu ya vyoo ingawaje amedai kuwa imekuwa ikifanya vizuri kwenye matokeo ya mitihani ya taifa kwa miaka mitatu mfululizo.

“Kutokana na mpango huu wa Equip-T, shule yetu imekuwa ikifanya vizuri sana kitaaluma kwa miaka mitatu mfululizo, haya ni mafanikio makubwa.”amesema mwalimu Masota huku akizungumzia hali ya miundo mbinu shuleni hapo “huwa inawalazimu wanafunzi kujisaidia kwa kupeana zamu wengine“.
Wadau wa elimu wilayani humo wamedai kuwa pamoja na changamoto hiyo shule hiyo inafanya vizuri kitaaluma na kushika nafasi tatu za juu kwa miaka mitatu mfululizo katika mitihani ya taifa.
Walimu katika shule hiyo nao wamesema kuwa katika kipindi cha mvua hali huwa mbaya zaidi shuleni hapo kwa kuwa choo wanachojisaidia huwa kinavuja na kuhatarisha usalama wao.
Hali hiyo ilibainika juzi baada ya timu ya wajumbe wa halmashauri hiyo pamoja na Waandishi wa Habari, wanaofuatilia simulizi ya mabadiliko ya elimu katika shule ambazo ziko kwenye mpango wa kuinua ubora wa elimu Tanzania (Equip-T).
Diwani wa kata ya Halawa, Andrew Enock, amesema katika kuchangia miradi ya maendeleo, lazima kila mtu awajibike ipasavyo na kwamba tayari wamekwishaweka mikakati kadhaa ikiwamo ya wananchi kuchangia kila kaya Sh. 10,000 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu zikiwamo nyumba za walimu na vyumba vya madarasa.
Mratibu wa Equip Tanzania, Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Isaya Adamu, amesema mpango huo  (Equip Tanzania) una malengo kupata maoni ya wadau wa elimu.
Chanzo:Nipashe na zanzibar24.

Comments